Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa timu ya Prisons, Fred Minziro ameeleza kuwa ratiba ya mechi zake imekuwa sababu kubwa ya kufanya vibaya kwenye michuano ya Ligi Kuu NBC msimu huu.
Minziro ameiambia GreenSports leo Ijumaa kuwa hajaridhishwa na ratiba inayopangiwa timu yake akichukulia mfano wa mechi tatu za mwisho wamecheza ndani ya siku nane katika mikoa mitatu tofauti.
“Hatujafanya vizuri lakini kuna sehemu ni kama ratiba inatukandamiza, sababu huwezi kucheza mechi tatu ndani ya siku nane, tumecheza na KMC tarehe 27 tukiwa Dar es Salaam kisha tukacheza na Geita (Gold) tukiwa Mbeya.
“Baada ya hapo tarehe 3 ikabidi tuifuate Kagera Sugar kwao, na wakati huo Kagera haina mchezo wowote, imepumzika muda mrefu kwao, sasa kulikuwa na ulazima gani wa kuwahisha mchezo kama huo?” Alihoji Minziro kocha wa zamani wa Yanga na Geita.
Minziro alisema kuwa uchovu wa mfululizo wa mechi hizo ambazo walipata pointi mbili pekee baada ya sare ya KMC na Geita kabla ya kufungwa na Kagera mabao 2-1, unachangia kuzorota kwa utendaji kazi wa wachezaji wake na kupelekea matokeo yasiyoridhisha.
Kocha huyo hata hivyo, alisisitiza kuwa sasa anakwenda kujipanga pia kurekebisha makosa machache aliyoyaona kuhakikisha wanaanza na ushindi katika mechi yao inayofuata dhidi ya Coastal Union, Novemba 23, mwaka huu ili kurejesha hali ya ushindani na matumaini ya kupambana.
Kwenye ligi hiyo inayoshirikisha jumla ya timu 16, Prisons kwa sasa inashika nafasi ya 14 baada ya kucheza mechi tisa.