Seville, Hispania
Real Madrid hatimaye imebeba taji la Copa del Rey ikiwa ni mara ya kwanza tangu mwaka 2014 baada ya kuilaza Osasuna mabao 2-1.
Katika mechi iliyopigwa jana Jumamosi kwenye dimba la La Cartuja mjini Seville, Real Madrid ilineemeka na mabao ya Rodrygo aliyefunga la kwanza dakika ya pili na la pili dakika ya 70 wakati bao pekee la Osasuna likifungwa na Torro katika dakika ya 58.
Vinicius Jr ambaye amerudi kikosi cha kwanza cha Real Madrid alionekana kuwa moto akitoa mchango mkubwa katika bao la kwanza na kwa muda mrefu alikuwa tishio kwa safu ya ulinzi ya Osasuna.
Osasuna ambao wanashiriki katika hatua ya fainali ya michuano hiyo kwa mara ya pili mfululizo waliiweka pagumu Real Madrid baada ya kusawazisha kabla Rodrygo hajawavuruga kwa bao la pili.
Sambamba na kubeba taji, Rodrygo pia aliweka rekodi ya kufunga bao la mapema mno katika mechi ya fainali ya michuano hiyo alipofunga bao la kwanza sekunde ya 106 baada ya mchezo kuanza ikiwa ni sekunde chache kabla ya kuingia dakika ya pili ya mchezo.
Mara ya mwisho katika fainali ya michuano ya kikombe bao kufungwa mapema namna hiyo ilitokea miaka 17 iliyopita.
Osasuna, iliungwa mkono na mashabiki wake zaidi ya 25,000 walioupamba mji wa Sevilla kwa rangi nyekundu wakiwa na matumaini makubwa ya kubeba taji la kwanza kubwa katika historia ya miaka 103 ya klabu hiyo lakini mambo hayakwenda kama matarajio yalivyokuwa.
Kwa upande wa Real Madrid ushindi huo ni kama umeituliza timu hiyo na sasa inajivunia rekodi ya kubeba taji hilo kwa mara ya 20 na mawazo rasmi yamehamia kwenye mechi yao ya keshokutwa Jumanne ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Man City.
Kimataifa Real Madrid kinara Copa del Rey
Real Madrid kinara Copa del Rey
Read also
