Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Simba SC, Juma Mgunda ameeleza kuwa wataingia kwa tahadhari kubwa pindi watakaposhuka kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, kuikabili Eagle FC katika mchezo wa hatua ya pili ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), kesho, Jumamosi.
Simba inaingia kwenye mechi hiyo ikiwa na kumbukumbu ya kuishia hatua ya nusu fainali ya kombe hilo msimu uliopita ilipofungwa na Yanga bao 1-0 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Mgunda, alisema kwamba utakuwa mchezo mgumu na hawatoidharau Eagle kwani ni timu ambayo itakuwa inahitaji matokeo ili kujitengenezea jina hivyo wataingia kwenye mchezo huo wakiwa na tahadhari zote.
“Hivi sasa tunaangalia zaidi mechi hii ili tufanikiwe kushinda na kusonga mbele, lengo letu ni kushinda mataji na hili litafanikiwa iwapo tutashinda kila mchezo ulio mbele yetu.
“Tunajua tunaenda kukutana na timu yenye malengo sawa na sisi, vijana wangu wanajua nini wanapaswa kufanya naamini hawataniangusha, lengo letu ni kushinda ili kuweka hai matumaini ya kupigania kombe hili,” alisema Mgunda.
Mgunda alisema kikosi chake kinaendelea vizuri na mazoezi japo kwenye mchezo huo wa kesho watawakosa wachezaji wawili, Nelson Okwa na Kibu Denis ambao wanaendelea kujiweka sawa baada ya kutoka kwenye majeruhi hivi karibuni.
Mbali na mechi hiyo, michezo mingine itakayochezwa kesho ni baina ya JKT Tanzania dhidi ya Biashara United kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo ambapo Majimaji wataikabili Kengold kwenye dimba la Majimaji, Songea wakati Mashujaa watapepetana na Pamba kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.
E4M FC na New Dundee watavurugana kwenye Uwanja wa Samora, Iringa na Afya FC watakuwa na kibarua mbele ya African Sports, Uwanja wa Vwawa wakati Nzega United itapambana na KFC FC Uwanja wa Samora na Geita Gold watawakaribisha Transit Camp kwenye Uwanja wa Nyankumbu, Geita.
Nao Ihefu watawaalika Mtama Boys kwenye Uwanja wa Highland Estate, Mbeya huku Kagera Sugar wakiwa wenyeji wa Buhare FC kwenye dimba la Kaitaba, Kagera.
Na Dodoma Jiji itaumana na TMA Stars kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma wakati huo Mbao FC watakuwa na kibarua dhidi ya Mapinduzi kwenye Uwanja wa Nyamagana, Mwanza, Ruvu Shooting nao wataoneshana ubabe na Ndanda kwenye Uwanja wa Uhuru, wakati Costal Union watakuwa nyumbani Mkwakwani, Tanga dhidi ya Tanga Middle.
Soka Simba kutoichukukia poa Eagle FC
Simba kutoichukukia poa Eagle FC
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
