Na mwandishi wetu
Benchi la ufundi la Simba limeeleza kufurahishwa na kuupongeza usajili uliofanywa hivi karibuni na mabosi wa timu hiyo kwa kuwa umekidhi haja ya kikosi na kuibua ari mpya ya upambanaji.
Hayo yameelezwa na kocha msaidizi wa timu hiyo, Selemani Matola akifafanua kuwa usajili huo umekwenda kuziba mapengo yaliyokuwa wazi na kukamilisha kikosi hicho ambacho kwa sasa kipo nchini Misri kwa ajili ya kambi ya maandalizi ya msimu ujao.
Mbali na hilo, Matola ameipongeza pia kamati ya usajili kwa kumleta kocha Zoran Maki akimsifia kuwa ni kocha anayefahamu nini kinapaswa kufanyika ndani ya kikosi hicho kwa maana ya mifumo na jinsi ya kuiunganisha timu.
“Tupongeze uongozi na kamati kwa kazi nzuri waliyoifanya mpaka sasa, kwa kuleta wachezaji stahiki na kuziba mapengo ndani ya kikosi kwa ajili ya msimu ujao, tulikuwa na mapungufu yanayoonekana na yasiyoonekana lakini sasa tuko kamili kwa maana ya kuwa na wachezaji wanaohitajika kwenye nafasi husika.
“Hata ujio wa kocha umekuwa na tija mno maana anafahamu Simba inahitaji nini kwa maana ya mifumo na falsafa za ufundishaji. Kwenye mazoezi tulianza taratibu lakini siku zinavyosogea wachezaji wanaonyesha matokeo makubwa, mpaka tukimaliza kambi tutakuwa tayari kabisa,” alisema Matola.
Simba ikiwa na wachezaji wake wapya iliowatambulisha hivi karibuni, imejichimbia Ismailia, Misri kwa zaidi ya wiki moja sasa ikijiandaa na michuano ya msimu ujao baada ya kufanya vibaya msimu uliopita, .
Tayari baadhi ya wachezaji hao wameshaanza kuonyesha makali yao kwa kufunga kwenye mechi zao mbili za kirafiki za hivi karibuni. Augustine Okrah alifunga walipoumana na Ismaily na mechi kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Pia Moses Phiri naye alifungua akaunti yake ya mabao alipofunga moja kwenye ushindi wa mabao 6-0 dhidi ya Al-Akhdood huku leo jioni wakitarajiwa kucheza mchezo mwingine dhidi ya Haras El Hodoud.
Wachezaji wengine wapya waliotua Simba ni Victor Akpan, Mohamed Outtara, Nassor Kapama, Habibu Kyombo huku ikiwongezea mikataba kipa wake, Aishi Manula na kiungo mkabaji, Mzamiru Yassin.
Afcon2024 Matola ajivunia usajili Simba
Matola ajivunia usajili Simba
Read also