London, England
Man City imepata pigo baada ya mshambuliaji wake tegemeo, Erling Haaland kuumia enka na kulazimika kutoka katika mechi na Bounermouth ingawa City ilitoka na ushindi wa mabao 6-1.
Na ingawa kuumia huko kumeibua hofu ya kumkosa mshambuliaji huyo katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumanne ijayo dhidi ya Young Boys ya Switzerland, kocha wa City, Pep Guardiola amewatuliza mashabiki wa timu hiyo.
Pep badala yake alisema kwamba alilazimika kumtoa mchezaji huyo kipindi cha kwanza katika mechi hiyo ya Ligi Kuu England au EPL kama tahadhari na ni mapema mno kuingiwa hofu ya kumkosa katika mechi na Young Boys.
“Amepata mshtuko kidogo kwenye enka, hatukutaka kumuweka katika hali hatarishi ndio maana tukamtoa, hakujiona yuko sawa, anaweza kurudi uwanjani Jumanne au hata Jumamosi,” alisema Pep.
Haaland alijikuta katika hali hiyo katika kipindi cha kwanza wakati akikimbia kwenye eneo la boksi na hadi sasa klabu yake haijasema ni enka ya mguu upi iliyomkwaza mshambuliaji huyo ambaye hadi sasa ameifungia City mabao 13 msimu huu.
Katika mechi hiyo nyota mpya wa timu hiyo, Jeremy Doku alicheza soka lililovutia na funga bao la kwanza wakati mengine yalifungwa na Bernado Silva aliyefunga mawili, Manuel Akanji, Phil Foden na Nathan Ake.
Mashabiki wana kila sababu ya kuwa na hofu na Haaland kwani ndiye aliyekuwa kinara wa mabao wa EPL msimu uliopita wa 2022-23 na pia aliiwezesha Man City kuweka rekodi kwa kumaliza msimu na mataji matatu ya EPL, FA na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Matokeo ya mechi za EPL Jumamosi hii ni kama ifuatavyo…
Fulham 0-1 Man Utd
Brentford 3-2 West Ham
Burnley 0-2 Crystal Palace
Everton 1-1 Brighton
Man City 6-1 Bournemouth
Sheff Utd 2-1 Wolves
Newcastle 1-0 Arsenal