London, England
Kocha mkuu wa Chelsea, Thomas Tuchel inadaiwa anataka kumsajili straika Robert Lewandowski wa Bayern Munich ili achukue nafasi ya Romelu Lukaku,
Mpango huo unadaiwa pia kuchangiwa kwa kiasi fulani na Lukaku mwenyewe ambaye ana shauku ya kurudi Inter Milan ikiwa ni baada ya kuvumilia kipindi kigumu katika Ligi Kuu England akiwa na Chelsea baada ya kucheza mechi 26 za ligi hiyo na kufunga mabao manane.
Habari za ndani zinadai kuwa mazungumzo yamefanyika baina ya Lukaku (29) na Chelsea huku Chelsea wakionyesha utayari wa kumruhusu mshambuliaji huyo Mbelgiji kuondoka katika klabu hiyo ingawa wanataka mgawo kufidia ada ya Euro 115 milioni waliyoitoa mwaka jana kwa ajili ya mchezaji huyo.
Utata pekee ambao unadaiwa kujitokeza katika mpango huo ni Inter kutokuwa tayari kulipa ada kubwa badala yake wanataka wamchukue mchezaji huyo kwa mkopo jambo ambalo linaifanya Chelsea kusita kuchukua uamuzi haraka.
Awali Chelsea ilikuwa tayari kumtoa Lukaku kwa ada kati ya Euro milioni 20 au 25 lakini kwa hali ilivyo sasa katika mipango yao wanaweza kuwa tayari kupunguza dau hilo ingawa hapo hapo kuna mjadala kuhusu malipo ya mshahara wa mchezaji huyo ambao unafikia Pauni 300,000 kwa wiki.
Chelsea katika mkakati wake wa msimu ujao imedhamiria kuimarisha safu yake ya ushambuliaji, awali walimtaka Erling Haaland lakini wakazidiwa ujanja na Man City ingawa pia tatizo lilichangiwa na mmiliki wa zamani wa timu hiyo, Roman Abramovich aliyebanwa na mamlaka za Uingereza akidaiwa kuwa na ukaribu na Rais wa Urusi Vladimir Putin ambaye anashutumiwa kwa kuivamia Ukraine.
Kwa upande wake kocha Tuchel anadaiwa kwa kipindi kirefu amekuwa akivutiwa na Lewandowski ambaye aliwahi kunukuliwa akizungumzia dhamira yake ya kuwa tayari kuondoka Bayern Munich huku ikiaminika kuwa anavutiwa na changamoto ya kucheza katika Ligi Kuu England.
Na ingawa Chelsea ndio wanaotajwa sana, zipo habari kuwa Barcelona nao wanamtamani Lewandowski huku ikidaiwa mazungumzo ya awali kati yake na klabu hiyo yalikwenda vizuri ingawa Barcelona wamekuwa wagumu kwenye fedha. Nje ya klabu hizo, klabu nyingine zinazodaiwa kuivizia saini ya Lewandowski licha ya kuwa ana miaka 33 sasa ni PSG na Man United.
Jambo ambalo linadaiwa kuzivutia klabu nyingi kwa Lewandowski ni uwezo wake wa kufunga mabao licha ya umri kusonga, kwa msimu wa 2021/22 ameifungia Bayern mabao 35 na kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Ujerumani maarufu Bundesliga. Pamoja na mafanikio hayo lakini tayari ameiaga klabu hiyo baada ya msimu akiamini haitomzuia kuhama kwa sababu tu ina uwezo wa kufanya hivyo.
Kimataifa Lewandowski asubiriwa Chelsea
Lewandowski asubiriwa Chelsea
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
