Munich, Ujerumani
Mshambuliaji wa Bayern Munich, Sadio Mane ameachana na timu hiyo na kujiunga na Al-Nassr ya Saudi Arabia ambayo pia anachezea nyota wa zamani wa Man United na Real Madrid, Cristiano Ronaldo.
Mane, (pichani) mshambuliaji wa zamani wa Liverpool, ameifungia Bayern mabao 12 katika mechi 38 za msimu wa 2022-23 huku akiwa katika msimu mgumu ulioandamana na majanga ya kuwa majeruhi.
Mchezaji huyo pia Aprili mwaka huu alijikuta akiwa gumzo kwenye vyombo vya habari akidaiwa kumpiga mchezaji mwenzake, Leroy Sane wakiwa kwenye vyumba vya kubadilishia nguo baada ya kupoteza mechi yao ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Man City.
Katika siku za karibuni, Mane mwenye umri wa miaka 31 amekuwa akihusishwa na mipango ya kuihama Bayern na ikaelezwa kwamba alikuwa akiwaniwa na timu za Saudi Arabia huku Bayern ikidaiwa kwamba imerudisha pesa ilizotumia kumnunua mshambuliaji huyo kutoka Liverpool mwanzoni mwa msimu wa 2022-23.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bayern, Jan-Christian Dreesen aliwahi kusema kwamba Mane ambaye pia aliwahi kuichezea Southampton hakuwa na msimu rahisi tangu ajiunge na timu hiyo akitokea Liverpool.
“Na ndio maana sote pamoja tumeamua kwamba afungue ukurasa mpya wa maisha yake ya soka na kuanza upya katika klabu nyingine, tunamtakia kila la kheri na mafanikio katika changamoto mpya na Al-Nassr,” alisema Dreesen.
Mapema leo Jumanne, kocha wa Bayern, Thomas Tuchel alisema kwamba yeye na Mane walikubaliana kwa pamoja kwamba kilichotokea hakikuwa kitu kizuri.
“Tulikumbatiana kwa muda mrefu na kwa pamoja tulikubaliana kwamba hatujapenda kilichotokea wakati huu lakini tunafikiri ni katika mazingira yaliyo mema,” alisema Tuchel.
“Kuna wakati mambo hayaendi vizuri kama ambavyo mtu anataka, mimi binafsi nimekuwa na uhusiano mazuri na Mane na itabaki kuwa hivyo, naelewa kabisa ameumizwa na hata mimi siwezi kufurahia mambo yakiwa katika namna hiyo,” aliongeza Tuchel.