Milan, Italia
Mtu mmoja ameuawa na wengine watano kujeruhiwa kwa kochomwa kisu akiwamo beki wa Arsenal, Pablo Mari katika tukio lililotokea kwenye Supermarket moja mjini Milan, Italia.
Akizungumzia tukio hilo, Mari ambaye kwa sasa anaichezea kwa mkopo klabu ya Monza inayoshiriki Ligi ya Serie A nchini Italia, alisema kwamba anajiona mwenye bahati kwa kukikwepa kifo baada ya kuchomwa kisu na kushuhudia mtu mmoja akiuliwa mbele yake.
Mtu aliyeuawa katika tukio hilo amefahamika kwa jina la Luis Fernando Rugierri ambaye ni mfanyakazi katika Supermarket hiyo, pamoja na mfanyakazi mwingine aliyejeruhiwa na wateja wengine wanne akiwamo Mari nao walijeruhiwa. Mari kwa sasa yuko hospitali na huenda akakosekana uwanjani kwa takriban wiki kadhaa.
Wakati tukio hilo linatokea Mari alikuwa ameandamana na mkewe na mtoto wao wa kiume na ghafla akachomwa kisu mgongoni na tayari mtu mmoja mwenye umri wa miaka 48 anayedaiwa kufanya unyama huo amekamatwa ingawa kwa sasa anatibiwa katika Hospitali ya San Paolo kitengo cha magonjwa ya akili.
Mtu huyo ambaye anadhaniwa kuwa na matatizo ya akili alichukua kisu kilichokuwa kikiuzwa kwenye Supermakket hiyo na kuanza kuwachoma watu hovyo kwenye eneo la supermarket hiyo ingawa hadi sasa polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.
“Baada ya tukio baya lililotokea jana, napenda kusema kwamba mimi na familia yangu kwa bahati tuko salama licha ya janga lililotukuta, na tunatuma salamu za rambirambi kwa ndugu na marafiki waliofiwa, na tunawaombea wote waliojeruhiwa wapone haraka,” alisema Mari jana Ijumaa kupitia mtandao wa Twitter, taarifa iliyoandamana na picha yake akiwa kwenye kitanda cha hospitali.
Habari zaidi zinadai kwamba mchezaji wa timu ya Napoli, Massimo Tarantino ni mmoja wa watu waliofanya juhudi kubwa hadi kufanikiwa kumnyang’anya kisu mtu aliyefanya ukatili huo. Mari alijiunga na Arsenal Januari 2020 akitokea Flamengo ya Brazil na kucheza mechi 19 na vigogo hao wa jiji la London kabla ya kuuzwa kwa mkopo katika klabu ya Monza.
Kimataifa Beki Arsenal achomwa kisu
Beki Arsenal achomwa kisu
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
