Na mwandishi wetu
Umahiri wa kiungo Clatous Chama umeendelea kuonekana katika Ligi Kuu NBC baada ya kutoa mchango mkubwa kwa Simba iliyoichapa Prisons mabao 4-0, mechi iliyochezwa Jumapili, Mei 10, 2026 kwenye Uwanja wa KMC, Mwenge, Dar es Salaam.
Ushindi huo umezidi kuiamsha Simba katika mbio za kulisaka taji la ligi hiyo wakichuana na mahasimu wao Yanga ambao ndio wanaoshika usukani wakiizidi Simba kwa tofauti ya pointi tano.
Simba sasa imefikisha pointi 49 katika mechi 22 ilizocheza wakati Yanga imeshakusanya pointi 54 ikiwa imecheza mechi sawa na za Simba.
Simba iliuanza mchezo kwa kasi ikiwa imedhamiria kutoa kichapo na katika dakika ya 12 timu hiyo ilipata penalti ambayo hata hivyo mpigaji, Seleman Mwalimu alipiga shuti lililoota mbawa.
Iliwachukua wachezaji wa Simba dakika 15 kuwasahaulisha mashabiki wao machungu ya kukosa penalti walipoandika bao la kwanza lililofungwa na Morrice Abraham aliyeuwahi mpira uliookolewa na mabeki wa Prisons.
Simba iliandika bao la pili dakika ya 42, bao lililofungwa na Chama kiufundi kwa kuunyanyua mpira juu wakati kipa wa Prisons, Mussa Mbisa akiwa ametoka katika eneo lake na kupishana na mpira huo.
Dakika moja kabla ya timu kwenda mapumziko Mwalimu alisahihisha makosa ya penalti aliyokosa kwakuipatia Simba bao la tatu, akitumia pasi ya Libase Gueye na kuifanya Simba iende mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 3-0.
Umahiri na ubora wa Chama ulijionesha tena katika dakika ya 62 alipoiwezesha Simba kupata bao la nne lililofungwa na Ismail Toure kwa kichwa kutokana na kona iliyochongwa na Chama.
Hii ni mara ya tatu mfululizo kwa Chama kuifungia Simba bao, baada ya kufanya hivyo katika mechi dhidi ya Yanga na JKT na hatimaye kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa mechi hiyo akifanya hivyo mara ya pili mfululizo.
Kimataifa Chama ang’ara Simba ikiilaza Prisons 4-0
Chama ang’ara Simba ikiilaza Prisons 4-0
Related posts
Read also
