Doha, Qatar
Kocha wa Qatar, Felix Sanchez amesema timu yake ipo tayari kucheza mechi yake ya kwanza ya fainali za Kombe la Dunia leo Jumapili katika tukio ambalo amesema litakuwa la kihistoria.
Qatar ambayo ni nchi mwenyeji wa fainali hizo watacheza mechi yao ya kwanza ya Kundi A dhidi ya Ecuador ambapo baada ya mechi hiyo, timu hiyo ambayo ipo nafasi ya 50 kwa mujibu wa viwango vya Fifa, itacheza na Senegal na Uholanzi ambazo zote zipo Kundi A.
“Ni siku muhimu mno kwetu, ni tukio la kihistoria, ni tukio la furaha kwetu,” alisema Sanchez mwenye umri wa miaka 46 ambaye anatokea Hispania.
“Ni siku ya aina yake isiyofanana na siku nyingine, tumefanya juhudi kubwa katika nchi hii, tumejitolea kwa ajili ya fainali hizi za Kombe Dunia, tumewekeza kwa kiasi kikubwa, naamini ni sherehe kubwa tunayoweza kuitumia kufurahia soka, natumaini kila mtu kutoka nchi nyingine zote anaweza kufurahia jambo hili, nina furaha kuwa wa kwanza kufungua michuano hii,” alisema Sanchez.
Sanchez pia alisema kwamba kucheza michuano hii ukiwa nyumbani mbele ya mashabiki wako kunafanya tukio hili kuwa la hadhi ya juu wakiwa wanafahamu fika wao ni kina nani, walipotokea na nani wanakutana naye.
Nahodha wa timu ya Qatar, Hassan Al-Haydos, ambaye anaichezea timu ya Al Sadd ya Doha alisema kwamba Qatar inajivunia na imejaa hamasa kwa kuanza kwa mashindano haya. “Hakuna heshima kubwa kama kucheza fainali za Kombe la Dunia, ni jukumu kubwa lakini tuko tayari, sina la kusema zaidi ya kujivunia kuongoza kikosi,” alisema mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31.
“Mashindano ya safari hii ya Kombe la Dunia ni kwa nchi za Arabuni, tuna jukumu kwa nchi zote za Kiarabu, kucheza vizuri na kuwa ana ari, tuna jukumu la kuwawakilisha Waarabu wote, mimi na wenzangu tutacheza kukidhi malengo na kudhihirisha matokeo ya juhudi zetu,” alisema.
Kwa upande wake kocha Sanchez katika mechi ya leo atakuwa na uamuzi wa kuchagua makipa wawili kati ya Saad Al Sheeb na Meshaal Barsham, ambao wote amekuwa akiwapanga katika mechi za kirafiki za timu hiyo mwaka huu.
Mshambuliaji Almoez Ali, ambaye amefunga mabao tisa na timu ya Taifa ya Qatar iliyotwaa Kombe la Asia mwaka 2019 bila shaka ndiye anayetarajia kuongoza safu ya ushambuliaji akishirikiana na Akram Afif, mtoto wa mchezji wa zamani wa timu ya Simba ya Tanzania, Hassan Afif.
Ecuador nayo itakuwa na ushindani katika nafasi ya kipa ingawa matarajio makubwa ni kwa kipa Alexander Dominguez mwenye rekodi ya kucheza mechi 459 bila kufungwa katika mechi za kimataifa ndiye atakayecheza mechi na Qatar.
Mchezaji mwingine muhimu wa timu hiyo, winga Romario Ibarra amekuwa akisumbuliwa na maumivu ya kidole aliyoyapata katika mechi ya kirafiki na Iraq ingawa hilo haliwezi kumkwaza hadi kushindwa kuiwakilisha Ecuador katika mechi ya leo.
Bado haijajulikana kwa kiungo mkabaji Carlos Gruezo ambaye hivi karibuni ilielezwa kwamba alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya misuli ya paja japo yapo matumaini ya kucheza mechi ya leo.
Swali ambalo mashabiki wanajiuliza ni je Qatar itavuka hatua ya makundi au itashindwa na kuaga michuano hiyo mapema kama ilivyokuwa Afrika Kusini mwaka 2010 ambayo ikiwa mwenyeji iliishia hatua ya makundi.
Kwa Qatar hii ni mara yao ya kwanza kushiriki fainali za Kombe la Dunia wakati kwa wapinzani wao Ecuador wanashiriki kwa mara ya nne.
Leo Jumapili Novemba 20, 2022
Qatar v Ecuador, saa 1:00 usiku
