London, England
Kocha wa Man United, Erik ten Hag amefurahishwa na mshambuliaji wake mpya, Wout Weghorst ambaye ameonyesha thamani yake kwa kufunga bao lake la kwanza na timu hiyo katika mechi ya Kombe la Carabao dhidi ya Nottingham Forest.
Katika mechi hiyo ya nusu fainali iliyochezwa jana Jumatano, Man United iliyokuwa ugenini ilitoka na ushindi wa mabao 3-0 huku Weghorst (pichani) mbali na kufunga bao moja lakini alicheza soka la kuvutia jambo lililomfurahisha Ten Hag.
Ten Hag alisema kwamba mchezaji huyo tangu atue katika klabu hiyo kwa mkopo akitokea Burnley, amekuwa na mchango wa kipekee ambao unaweza usionekane ikiwamo kuwatengenezea wenzake nafasi za kufunga.
Akilizungumzia bao la Weghorst, Ten Hag alisema kwamba, mchezaji huyo Mholanzi ameonyesha kuwa na jicho la goli baada ya kuuwahi mpira uliopigwa na Antony na kutemwa na kipa Wayne Hennessey na kuujaza wavuni muda mfupi kabla ya timu kwenda mapumziko.
“Amefunga bao ni muhimu kwake na kumfanya awe mwenye kujiamini zaidi, alifanya kazi nzuri katika mechi dhidi ya timu za Crystal Palace na Arsenal kwa pasi, kujipanga vizuri na kuendanana kasi ya mchezo,” alisema Ten Hag.
“Alisaidia bao la Bruno (Fernandez) katika mechi na Palace kwa sababu alikuwa akienda vizuri na kasi ya mchezo akiwa mbele, pia alichangia bao la Rashford katika mechi na Arsenal kwa sababu aliwahadaa mabeki,” alisema Ten Hag.
Ten Hag alisema kwamba kwa bao alilofunga, Weghorst atakuwa mwingi wa furaha kwa sababu washambuliaji wapo kwa ajili ya kufunga mabao na wanapokosa kufunga wanakosa furaha.