Na mwandishi wetu
Kaimu kocha mkuu wa Simba SC, Juma Mgunda ameweka wazi kuwa hajakata tamaa ya kuwania taji la Ligi Kuu NBC msimu huu kwa kuwa msimu bado haujamalizika na hakuna aliyejihakikishia ndoo hiyo mpaka sasa.
Mgunda ameeleza hayo baada ya ushindi wa mabao 2-0 walioupata jana dhidi ya Mtibwa Sugar, ambapo Wekundu hao wameendelea kusalia nafasi ya tatu kwa pointi 50.
Simba wapo nyuma ya Azam wanaoshika nafasi ya pili wakiwa na pointi 54 na vinara wa ligi hiyo Yanga wenye pointi 62, lakini Simba ikiwa na mchezo mmoja mkononi.
“Tunashukuru kwanza mchezo ulikuwa mzuri na wenye ushindani na haikuwa rahisi kama inavyofikiriwa, tumepata alama tatu, tunajipanga na mchezo mwingine.
“Na kuhusu ubingwa niseme ni kama marathon, huwa unapatikana pale mbio zinapoisha ila kwa sasa kuna anayeongoza, anayefuata nyuma, sasa yule atakayekata utepe mwisho ndio bingwa.
“Kwa hiyo bado tupo kwenye mbio, tunaangalia kilicho mbele yetu na michezo iliyo mbele yetu tunatazamia kufanya vizuri kwenye mechi zilizobaki kisha tutaangalia tumesimamia wapi, yaani maana yake ni kwamba haiishi mpaka iishe, mpaka ifike mwisho ndio tutaamini sasa imwekwisha,” alisema Mgunda kocha wa zamani wa Coastal Union.
Mgunda ambaye amerithi mikoba ya Abdelhak Benchikha ameeleza kuwa ameanza vizuri katika timu hiyo baada ya mechi iliyopita kupata sare ya mabao 2-2 na Namungo na hiyo inatokana na uwepo wa kocha msaidizi, Selemani Matola ambaye amewahi kufanya naye kazi Simba pia siku za nyuma, hivyo kazi yake inakuwa rahisi kwa kuwa wanajuana vizuri kikazi.