Manchester, England
Kocha wa Manchester United, Erik ten Hag amethibitisha mshambuliaji wake, Marcus Rashford kuongeza mwaka mmoja katika mkataba wake na klabu hiyo.
Mbali na Rashford ambaye iliwahi kuelezwa kuwa anatakiwa na klabu ya PSG ya Ufaransa, Man United pia imewaongezea mkataba wa mwaka mmoja mmoja wachezaji wengine Diogo Dalot, Fred na Luke Shaw ambao kama Rashford nao walikuwa katika mwaka wa mwisho wa mikataba yao na wana kipengele kinachowapa fursa ya kuongeza tena mkataba katika kipindi cha miezi 12.
Rashford ameonekana kuwa katika kiwango bora msimu huu chini ya Ten Hag akiwa hadi sasa tayari amecheza mechi 20 za mashindano mbalimbali na kufunga mabao tisa wakati Dalot, Fred na Shaw pia wamehusika kwa kila mmoja wao kucheza mechi 15 za mashindano mbalimbali.
“Ndio naweza kuthibitisha hilo,” alisema Ten Hag katika taarifa yake iliyopatikana kwenye mtandao wa klabu hiyo.
“Tuna furaha kwa sababu kikosi kinakwenda katika mwelekeo mzuri na wachezaji hao wana mchango mkubwa katika mwelekeo huo, tunataka kuwaendeleza na kuwaunga mkono wachezaji hao na tunataka wawemo katika mpango wetu,” alisema Ten Hag.
“Kwa hiyo wanatokana na maamuzi hayo, nina hakika ni maamuzi sahihi, tunataka kujenga timu ya baadaye, timu ya miaka mingi ijayo na hao wachezaji wanatakiwa kuwa sehemu ya mpango huo,” aliongeza Ten Hag.
Kipa namba moja wa timu hiyo, David de Gea ambaye pia yuko katika mwaka wa mwisho wa mkataba wake naye ana fursa ya kuongeza mkataba lakini bado hajafikia makubaliano na klabu ingawa tayari Ten Hag aliwahi kusema miezi miwili iliyopita kwamba kipa huyo Mhispaniola atabaki katika klabu hiyo ya Old Trafford.
