Na mwandishi wetu
Mgombea pekee wa nafasi ya urais wa klabu Yanga, Injinia Hersi Said leo ameweka wazi nia iliyomfanya agombee nafasi hiyo pamoja na kuainisha vipaumbele vyake.
Mgombea huyo amezungumza hayo akiwa ameambatana na mgombea wa nafasi ya makamu wa rais, Arafat Haji ambaye anachuana na Suma Mwaitenda.
Hersi ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano klabu hiyo na Mkurugenzi wa Uwekezaji GSM amejinasibu kwenye vipengele vya kukamilisha mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji wa klabu na miundombinu kwa maana ya ujenzi wa uwanja wao wa Kaunda uliopo mitaa ya Twiga na Jangwani, Kariakoo jijini Dar es Salaam.
“Ni wakati muafaka sasa baada ya mwenyekiti wetu wa Kamati ya Uchaguzi (Malangwe Mchungahela) kuzindua rasmi kampeni. Kwa kutumia fursa hiyo na mimi nazindua kampeni nikiambatana na Arafat Haji, hili ni tukio maalum kwake pia kwa kuwa naye anagombea umakamu wa rais.
“Machache ambao yamenifanya kuomba nafasi ya kuingoza yanga, kwanza wote mnafahamu jiihada zangu binafsi lakini jitihada za kamati yetu ya mabadiliko kuhakikisha kwamba tunatoka kwenye mfumo wa kizamani na kwenda mfumo mpya wa uendeshaji.
“Napenda niwahakikishie wanachama na mashabiki wa Yanga mimi ni muumini mkubwa wa mabadiliko yale, niwahakikishie nikipewa nafasi ya kuwa rais wa klabu hii nitakwenda kuyaenzi, kuyaendeleza na kusimamia mabadiliko hayo kivitendo.
“Kipaumbele changu kingine nikipata nafasi ni miundombinu, Yanga ndiyo kongwe nchini, tunaweza kujivunia kwa yaliyotokea nyuma lakini ni aibu kujifahari kwa ukongwe wa klabu na kukosa miundombinu sahihi,” alisema Hersi.
Kupitia hilo, Hersi alisisitiza kuwa tayari ameshafanya hesabu za ukubwa na namna ya kuujenga uwanja wa Kaunda kwa ajili ya kuingiza mashabiki 20,000 ambao ndiyo wastani wa mashabiki wanaoingiza kwenye mechi zao nyingi za msimu na hivyo hiyo inaweza kuwasaidia mno.
“Ninawaahidi Wanayanga nitaanzisha mchakato wa kujenga uwanja wenye uwezo wa kuingiza watu 20,000 eneo la Kaunda. Kaunda inatosha idadi hiyo, hii hesabu nimeitoa kwenye uhalisia wa idadi ya wastani ambao mashabiki wanakuja kwenye mechi zetu ukitoa tukicheza na Simba na Azam.
“Wastani unacheza kuanzia mashabiki 8,000 mpaka 12,000 ikizidi 15,000. Tukiweza kubeba watu hao tutaweza kubeba mechi zetu za ligi kwa asilimia 85 mpaka 90. Tunajenga hapo kwa ajili ya eneo tulilopo ambalo ni katikati ya mji na rahisi kufikika,” alisema Hersi.
Pia, Hersi aligusia mipango mingine mingi ya mradi wa uwanja wao wa Kigamboni na namna atakavyoboresha jengo la makao makuu la klabu hiyo akilisifia kuwa limekaa kisasa ingawa lilijengwa muda mrefu na vitu vingi ni vya kuboresha kwa sababu vilishajengwa na wazee wa zamani wa timu hiyo.
Mchakato wa kampeni za uchaguzi huo zilianza rasmi jana na zitadumu kwa takriban siku tano kabla ya Julai 9 mwaka huu siku ambayo utafanyika uchaguzi huo kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.
Soka Hersi aanika vipaumbele vyake Yanga
Hersi aanika vipaumbele vyake Yanga
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
