Barcelona, Hispania
Beki wa zamani wa timu ya taifa ya Brazil na klabu ya Barcelona, Dani Alves anayetumikia kifungo cha miaka minne na nusu jela kwa kosa la kubaka msichana, anaweza kutoka jela baada ya kutumikia robo ya adhabu inayomkabili.
Mwezi uliopita Alves alihukumiwa kifungo hicho na mahakama moja mjini Barcelona kwa kosa la kumbaka msichana katika klabu ya usiku mjini Barcelona, kosa analodaiwa kulifanya usiku mmoja wa Desemba, 2022.
Alves, 40, amekuwa kifungoni tangu Januari 2023 baada ya kunyimwa dhamana wakati wote wa kesi hiyo kwa hofu kwamba angeweza kutoroka, sasa anaweza kuwa nje ya gereza kwa malipo ya dhamana ya Pauni 852,500
Masharti mengine ya dhamana ambayo mchezaji huyo amepewa ni kuzikabidhi mamlaka husika hati zake za kusafiria za Brazil na Hispania ili asiweze kuondoka nchini Hispania.
Katika masharti hayo Alves pia atatakiwa kuripoti mahakamani kila wiki na kutomsogelea kwa karibu msichana anayedaiwa kumbaka, masharti ambayo wakili wa mchezaji huyo ameyataja kuwa ni mfano wa kashfa.
Mahakama hiyo imefikia uamuzi huo baada ya maombi ya wakili wa Alves kutaka mteja wake aachiwe kwa kuwa tayari ametumikia robo ya adhabu yake kwa kuwekwa kifungoni tangu akamatwe Januari mwaka jana.

Akifafanua hoja yake kuhusu uamuzi wa mahakama, wakili wa Alves alisema kwamba ni mfano wa kashfa kwa sababu mahakama imefikia uamuzi wa kutaka kiasi hicho cha fedha ili imuachie mshtakiwa kwa kuwa inaamini ni mtu anayeweza kupata mamilioni ili atoke kifungoni.
Alisema kwamba kilichofanywa na mahakama hiyo ni sawa na kuwa na utaratibu wa kutoa haki matajiri wenye uwezo hivyo anajipanga kwa ajili ya kuukatia rufaa uamuzi huo.
Siku ambayo tukio la ubakaji linadaiwa kufanywa, Alves akiwa katika klabu hiyo ya usiku anadaiwa kuwanunulia pombe kali wasichana watatu na baadaye kumrubuni mmoja na kumpeleka eneo la VIP ambalo lina choo.
Inadaiwa wakiwa eneo hilo, Alves alibadilika ghafla na kuwa mbabe kwa kumlazimisha msichana huyo kufanya naye ngono licha ya msichana huyo kumkatalia lakini alitumia nguvu kufanikisha tukio hilo.
Katika utetezi wake Alves alidai kwamba msichana huyo angeweza kuondoka kama angetaka lakini mahakama iliona kuna utumiaji nguvu uliofanywa na mchezaji huyo katika kufanikisha tukio zima.
Mahakama ilielezwa kuwa Alves alimshika kwa nguvu msichana huyo na kumungusha chini kabla ya kutekeleza tukio la ubakaji kwa msichana huyo mwenye umri wa miaka 23 ambaye anasema alichofanyiwa na Alves kimemsababishia madhara makubwa.
Alves hata hivyo alionekana kujichanganya mara kadhaa katika utetezi wake, awali alikana kumjua msichana aliyemshitaki na kwamba alimuona mara ya kwanza chooni na hakumfanyia jambo lolote msichana huyo.
Baadaye alidai kuwapo makubaliano kati yake na msichana huyo na kwamba walifurahia tukio zima kwa pamoja lakini baada ya hapo alisema alifanya alichomfanyia msichana huyo kutokana na ushawishi wa pombe na kuitaka mahakama isimpe adhabu kali.
Mbali na Barcelona ambayo aliichezea kwa mafanikio zaidi kwa kubeba taji la La Liga mara sita, Ligi ya Mabingwa Ulaya mara tatu, Alves pia amewahi kuzichezea timu za Sevilla, Juventus, PSG na ni kati ya wachezaji walioichezea mara nyingi timu ya taifa ya Brazil, mara 126.
