Barcelona, Hispania
Beki wa zamani wa timu ya taifa ya Brazil na klabu ya Barcelona, Dani Alves anadaiwa kuiambia mahakama kwamba siku aliyotuhumiwa kumfanyia mwanamke udhalilishaji kijinsia alikuwa amelewa.
Kauli ya mchezaji huyo imekuja wakati kesi inayomkabili ikitarajia kuanza kusikilizwa mwezi ujao na kwa sasa bado yuko ndani baada ya kunyimwa dhamana kwa hofu kwamba anaweza kukimbia.
Madai ya mchezaji huyo kwamba alikuwa amelewa yanaweza kumfanya apunguziwe adhabu kama akikutwa na hatia ya kosa analotuhumiwa kulifanya.
Kwa mujibu wa mwanasheria mmoja anayedaiwa kuwa karibu na mchezaji huyo, kiwango cha pombe ambacho Alves alikunywa kilikuwa cha juu na kilimfanya awe katika hali ya kutojua matendo aliyokuwa akiyafanya.
Kauli ya sasa ya mchezaji huyo inaweza kuonekana kama ni ya kujichanganya kwani hapo awali mara zote alikuwa akikana kufanya kosa analotuhumiwa na wala hamjui mwanamke anayemtuhumu.
Pia amewahi kusema kwamba alikutana na mwanamke huyo eneo la maliwato lakini hakuna chochote kilichotokea baina yao, hapo hapo aliwahi kusema kwamba kuna tukio la kugusana baina yao na sasa anadaiwa kuibuka na habari mpya ya kuzidiwa na ulevi.
Mara ya kwanza mchezaji huyo alihusishwa na tuhuma hizo Desemba 2022 na kukamatwa Januari mwaka 2023 akituhumiwa kumdhalilisha mwanamke katika klabu moja ya usiku mjini Barcelona.
Baada tu ya kuhusishwa na tuhuma hizo, beki huyo ambaye pia amewahi kuichezea PSG, mkataba wake na klabu aliyokuwa akiichezea ya Pumas Unam ya nchini Mexico ulisitishwa.
Kimataifa Alves aitaja pombe kwenye kesi ya udhalilishaji
Alves aitaja pombe kwenye kesi ya udhalilishaji
Read also