Na Abdul Mohammed
Jumamosi moja tulivu, mwaka 2011 au 2012, saa nne au tano asubuhi, niko chuoni UCU (Uganda Christian University) mjini Mukono, Uganda kwenye hosteli ya wanafunzi wanamichezo kuanzia soka, kikapu, wavu, rugby, riadha na wengineo.
Kwa kawaida huo ni muda ambao wanafunzi tuliutumia kufanya usafi, iwe kuosha vyombo, kusafisha vyumba, kufua nguo huku nyimbo za wasanii tofauti zikisikika kwa wanafunzi wengi wao wakiwa ni kutoka Kenya, Tanzania, Rwanda, Sudan Kusini na wenyeji Uganda.
Hapo utawasikia kina Khaligraph, Chameleon, Mr Nice, Diamond, Ali Kiba na wengineo sambamba na mijadala katika makundi tofauti tofauti ikiendelea, kuanzia mijadala ya masomo, michezo, pombe, starehe za Ijumaa usiku na mengineyo.
Mjadala ulionivutia ni ule wa wachezaji wa timu ya kikapu ya UCU Canon waliokuwa wakijiandaa kwa mechi ya ligi dhidi ya Falcon pale mmoja wao alipouliza. “Sasa nani atashika Dulla?
Niliposikia jina la Dulla nilimkumbuka nyota wa kikapu nchini Abdallah Ramadhan na nilipomuuliza mwanafunzi kutoka Kenya ambaye alikuwa akishiriki katika mjadala ule aliniambia ndio huyo huyo wakati huo Dulla alikuwa akichezea timu ya Falcon.
Mwanafunzi yule ambaye naye alikuwa mchezaji wa UCU Canon akaanza kumchambua Dulla. “Aaah acha tu jamaa ni Mu-aggressive (nafikiri alimaanisha mpambanaji au msumbufu uwanjani).
Kwa sasa Dulla yuko nchini Tanzania na licha ya kuwa na miaka 47 lakini mapenzi na uwezo wake katika mchezo wa kikapu vyote vinajidhihirisha waziwazi katika mazungumzo niliyofanya naye.
Jambo linaloweza kushangaza wengi ni kwamba pamoja na umri huo bado anacheza mpira wa kikapu akiwa na timu ya Pazi na si Vijana aliyokuwa akiichezea miaka ya nyuma kabla ya kutimkia Seychelles na baadaye Uganda.
Moja ya mambo yanayomnyima raha ni namna ambavyo mpira wa kikapu Tanzania unaendelea katika namna ya kusuasua, hamasa iko chini hasa anapolinganisha na Uganda alikokuwa akicheza kama mchezaji profesheno na kwingineko.
Na moja ya sababu anayoona inachangia hali hiyo ni kukosekana utaratibu mzuri wa kukuza vipaji kutoka chini na matatizo ya viongozi wenye dhamana ya mchezo huo.
Hapo hapo anarudi nyuma miaka ya 1990 mwishoni na 2000 mwanzoni na kukumbuka namna ambavyo ushindani wa timu za Pazi na Vijana ulivyokuwa juu katika mpira wa kikapu kuanzia jijini Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla.
“Wote mliokuwa mkituona wakati ule tukishindana na kucheza kwa kiwango cha juu tulitokea shule, vipaji vyetu vilionekana tukiwa shule tunashindana kwenye UMISETA (michezo ya shule za sekondari) hii michezo ilipotea kwa kipindi kirefu,’’ anasema Dulla.
Katika maendeleo ya mpira wa kikapu, Dulla anaiangalia na kuitolea mfano Rwanda akizungumzia mafanikio ambayo nchi hiyo imeyapata kupitia mpira wa kikapu.
Anakumbuka wakati wakienda Rwanda na kucheza kwenye Uwanja wa Amahoro ambao eneo la kuchezea mpira wa kikapu lilikuwa hovyo, halina hadhi lakini sasa wana uwanja wenye hadhi kama ya viwanja vya nchini Marekani.
“Leo hii timu ya kikapu kutoka Marekani ikitaka kufanya ziara za kabla ya msimu (pre-season) wataichagua Rwanda si Tanzania, kwa sababu Rwanda wao wana uwanja wenye hadhi hapa kwetu hatuna, sasa inakuwaje tunashindwa hata na Rwanda?” Anahoji Dulla huku akionyesha kushangaa na kuongeza kuwa nchi inajinyima fursa za kupata wageni kutoka nje.
Dulla anaamini kwamba Tanzania inaweza kufikia hatua hiyo na kufaidika na ujio wa timu za Marekani na kwingineko kinachohitajika ni uwekezaji.
Anasema kwamba huwezi kuendeleza mpira wa kikapu wakati hata uwanja wa kufundishia vijana huna, “Unajua huu ni mchezo wa kasi sasa ni lazima mchezaji aandaliwe ili kuendana na kasi ya mchezo, maandalizi hayo yanahitaji viwanja vyenye sifa zinazohitajika.”
Akifafanua zaidi kuhusu maendeleo ya mpira wa kikapu nchini, Dulla anauangalia uchaguzi wa Shirikisho la mchezo huo nchini unaotarajia kufanyika baadaye mwaka huu, na kusisitiza kuwa ni lazima waingie viongozi wenye nia ya kuleta maendeleo ya mpira wa kikapu.
“Nimesikia habari ya uchaguzi na kuna wenye nia ya kuwania uongozi, sisi tunataka maendeleo, wasimame watu wenye nia safi, waingie watu wa kusaka vipaji kwani vipo na vinahitaji kuendelezwa,” anasema Dulla na kusisitiza kuwa hana nia ya kuwania uongozi lakini anachopenda ni kuona maendeleo katika mpira wa kikapu.
Hapo hapo anamkumbuka Mbamba Uswege (marehemu) aliyekuwa kiongozi wa Chama cha Mpira wa Kikapu Dar es Salaam (DARBA) kuwa ni mtu aliyefanya kazi kubwa ya kuuweka juu mpira wa kikapu.
“Huo ni wakati ambao watu walikuwa wakiisubiri kwa hamu mechi ya kikapu hasa Vijana na Pazi, mechi zilikuwa zikionyeshwa kwenye televisheni mara kwa mara, hamasa ilikuwa juu,’’ anasema Dulla.
Anawakumbusha viongozi watakaoingia madarakani kuliangalia jambo hilo lakini pia walifanyie kazi suala zima la kuwa na uwanja wao kwani ni aibu kwa Tanzania kutokuwa na uwanja wa mpira wa kikapu wenye hadhi kama ilivyo Rwanda.
Anasema kwamba ni vizuri viongozi kutafuta wadhamini lakini hapo hapo anatadharisha kuwa hakuna mtu atakayetoa udhamini halafu baadaye akasikia mambo tofauti na yale anayoyataka halafu aendelee kutoa udhamini.
Aliingiaje kwenye kikapu
Kama ilivyo kwa vijana walio wengi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kutekwa na mapenzi ya soka, Dulla naye hakuwekwa kando na mkumbo huo, alikuwa akicheza soka na wenzake lakini akajikuta akiwa katika mabishano na baba yake.
“Unajua zamani nikiwa mdogo kule Zanzibar nilikuwa nikicheza soka na wenzangu, nilikuwa nacheza nafasi ya golikipa na baadaye kiungo lakini baba alinitaka niachane na soka na kucheza mpira wa kikapu.”
Dulla anasema suala hilo lilikuwa gumu mno kwake, alikataa licha ya juhudi za baba yake kumnunulia mikanda ya video ya mastaa wa kikapu wa Marekani kina Michael Jordan, Shaquile Oneil na wengineo pamoja na kumnunulia vifaa vya mchezo huo ili aachane na soka lakini Dulla alionekana kuwa mgumu.
“Unajua baba alikuwa mlezi wa timu ya kikapu ya Rangers ya kule Zanzibar sasa akawa anataka na mimi niingie katika timu hiyo nilimkatalia lakini baadaye nikaona sina sababu ya kushindana na mzee wangu Mwenyezi Mungu amrehemu, nikajikita kwenye mpira wa kikapu,’’ anasema Dulla.
Kilichomtokea Dulla kwa baba yake kimejirudia tena kwani mtoto wa kwanza wa Dulla anacheza soka ni golikipa, alijaribu kumuingiza kwenye kikapu kama yeye alivyofanyiwa na baba yake lakini ikashindikana japo anafarijika kwa kuwa mtoto wake wa pili anacheza mpira wa kikapu.
“Mtoto wangu wa pili anacheza mpira wa kikapu, wa kwanza nilijaribu kumtoa kwenye soka kama baba yangu alivyonitoa kwenye soka lakini kwangu ilishindikana,’’ anasema Dulla.
Dulla ni baba wa watoto watatu aliozaa na mkewe, Begethr Fortain ambaye ni raia wa Seychelles na jambo la kufurahisha ni kwamba mkewe naye ni mchezaji wa mpira wa kikapu ambaye amechezea timu ya Taifa ya Seychelles.