Penzi la Pique, Shakira njia panda
Mwaka 2010 Hispania ilibeba taji la Dunia nchini Afrika Kusini, nje ya mafanikio hayo kulikuwa na wapenzi wawili waliokuwa gumzo, beki wa timu hiyo Gerard Pique na mpenzi wake Shakira.
Wakati Hispania ikitamba duniani, wimbo wa Wakawaka uliokarabatiwa na Shakira nao ulikuwa gumzo duniani, ukipamba mafanikio ya timu hiyo na michuano ya Kombe la Dunia kwa ujumla.
Penzi la Shakira na Pique wakati huo lilikuwa moto kwa mambo mengi achana na umri, Shakira ana miaka 45 amemzidi Pique miaka 10, hapo usemi wa age is just a number ulishika hatamu, lakini wawili hao pia wanafurahia siku moja ya kuzaliwa, wote walizaliwa Februari 2, Pique 1987 na Shakira 1977.
Ni wakati ambao wawili hao walikuwa juu, penzi lao lilitajwa kuwa moja ya super couples, wote walikuwa juu, Shakira akitamba kwenye muziki na Pique akitamba kwa mafanikio kwenye timu ya Taifa ya Hispania na klabu yake ya Barcelona.
Kilichokuwa kikisubiriwa ni siku yao ya kufunga ndoa na kuwa mume na mke lakini wakati yote hayo yakiendelea ilidaiwa kwamba kuna mnajimu mmoja aliyewahi kunukuliwa akisema kwamba uhusiano wa wawili hao hauwezi kudumu, utavunjika tu.
Pamoja na mapenzi hayo motomoto, wawili hao hawakuwahi kufunga ndoa licha ya kupata watoto wawili Milan na Sasha na inadaiwa kwa sasa mambo yao hayako sawa, kila mmoja ameshika lake, mapenzi moto moto ya miaka 12 sasa yako njia panda.
Habari za ndani zinadai kwamba kwa sasa wawili hao hawakai nyumba moja, Pique ameamua kuondoka katika mjengo badala yake anaishi kwenye nyumba nyingine akidaiwa kuishi maisha ya ubachela mjini Barcelona.

Majirani wanadai kumuona akiingia na kutoka katika nyumba hiyo ya kupanga na zaidi ya hilo kuna habari kwamba amekuwa akifurahia maisha ya usiku katika jiji la Barcelona na kundi la marafiki zake wakati mwingine akirudi kwake usiku mnene.
Dalili nyingine kubwa ya wawili hao kutengana ni mashairi yaliyo katika kibao kipya cha Shakira kiitwacho Te Felicito. Katika mashairi hayo Shakira anasikika akiimba “For completing you I broke into pieces; they warned me, but I did not pay attention. Shakira hapo ni kama vile analalamika jinsi alivyojali lakini akaumizwa, jinsi alivyotahadharishwa lakini hakusikiliza (tafsiri isiyo rasmi).
Katika mashairi mengine Shakira anasema…”My eyes are red from crying so much for you; and now, it turns out that you are sorry; it sounds sincere, but I know you well and I know that you lie; I congratulate you, how well you act.” Na hapo ni kama vile anasema, macho yangu yamekuwa mekundu kwa sababu ya kulia sana, na sasa inaonekana kama unataka msamaha, unaonekana muungwana lakini nakujua na najua unaongopa, nakupongeza jinsi inavyoigiza vizuri (tafsiri isiyo rasmi).
Habari nyingine pia zinadai kwamba kitendo cha Pique kuhama katika mjengo aliokuwa akiishi na Shakira kimekuja baada ya Shakira kumfumania na mwanamke mwingine ambaye awali ilidaiwa ni mama wa mmoja wa wachezaji wa Barcelona lakini baadaye ikabainika hilo halikuwa kweli.
