Na mwandishi wetu
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Soka ya Wanawake, JKT Queens wamepangwa Kundi A katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji wa michuano hiyo, Athlético d’Abidjan ya Ivory Coast.
Timu nyingine zilizopangwa kundi moja na JKT ambayo inashiriki Ligi ya Mabingwa kwa mara ya kwanza msimu huu ni Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na Sporting Casablanca ya Morocco.
Katika droo hiyo iliyopangwa Abidjan, Ivory Coast Kundi B linazikutanisha timu za Ampem Darkoa ya Ghana, Huracanes ya Ghana, AS Mande ya Mali na mabingwa watetezi wa michuano hiyo, AS FAR ya Morocco.
JKT imefanikiwa kushiriki michuano hiyo baada ya kuibuka bingwa wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) ikiifunga CBE ya Ethiopia kwa penalti 5-4 baada ya suluhu ya dakika 90 Uwanja wa Njeru, Jinja nchini Uganda.
Mbali na ubingwa huo, JKT ilitajwa kutoa mchezaji bora, Stumai Abdallah na kipa bora, Najiath Idrissa kwenye michuano hiyo.
Huu ni msimu wa tatu kufanyika Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake na JKT inakuwa timu ya pili Tanzania kushiriki ligi hiyo baada ya Simba Queens iliyoshiriki msimu uliopita. Mamelodi ilikuwa ya kwanza kutwaa ubingwa huo ambao msimu uliopita ulichukuliwa na AS FAR.
Soka JKT Queens yapangwa na wenyeji Ligi ya Mabingwa
JKT Queens yapangwa na wenyeji Ligi ya Mabingwa
Read also