Doha, Qatar
Baada ya Argentina kukubali kichapo cha mabao 2-1 mbele ya Saudi Arabia jana Jumanne, Ujerumani nao leo Jumatano wamekutana na kipigo kama hicho mbele ya Japan kwenye fainali za Kombe la Dunia.
Japan ambayo ilikuwa nyuma kwa bao moja kwa kipindi kirefu ilifanikiwa kubadili matokeo katika dakika za 75 na 83 na kutoka uwanjani kifua mbele katika matokeo mengine yanayoibua sintofahamu juu ya nafasi ya vigogo hao katika fainali za mwaka huu za Kombe la Dunia zinazoendelea, Qatar.
Ujerumani iliandika bao lake la kwanza katika dakika ya 33 ya mchezo huo kwa mkwaju wa penalti uliojazwa wavuni na nyota wa Man City, Ilkay Gundogan baada ya Shuichi Gonda kumsukuma David Raum kwenye eneo la penalti.
Baada ya bao hilo, Ujerumani yenye timu iliyosheheni vijana na iliyopewa matumaini makubwa ya kufanya vizuri katika fainali za mwaka huu, ilifanikiwa kuutawala vyema mchezo huo na kutoa dalili zote za kutoka uwanjani na ushindi mnono.
Mambo hata hivyo yalianza kuwaharibikia Ujerumani, mabingwa hao mara tano wa dunia katika dakika ya 75 baada ya Ritsu Doan kuisawazishia Japan bao na dakika nane baadaye, Takuma Asano aliyeingia kipindi cha pili aliwainua mashabiki wa Japan kwenye viti baada ya kuandika bao la pili.
Ujerumani ambao mwaka 2014 walitwaa taji la dunia nchini Brazil, mambo yaliwaendea hovyo kwenye fainali za mwaka 2018 nchini Urusi baada ya kuaga katika hatua ya awali na sasa baada ya kufungwa na Japan tayari kuna wanaohoji nafasi ya timu hiyo kama itaweza kufika.
Ujerumani sasa inasubiri kuumana na Hispania katika mechi nyingine ya Kundi E ambayo inatarajia kuwa ngumu na baada ya hapo itamalizia mechi zake za makundi dhidi ya Costa Rica.
Wakati mambo yakiwaharibikia Ujerumani, Hispania ilifanya kweli baada ya kuipa Costa Rica kichapo cha mbwa koko kwa kuilaza mabao 7-0 huku mabao ya washindi hao yakifungwa na Olmo, Asensio, Torres aliyefunga mawili, Gavi, Soler na Morata.
Matokeo ya mechi za Kombe la Dunia…
Kundi A
Senegal 0-2 Uholanzi
Qatar 0-2 Ecuador
Kundi B
England 6-2 Iran
Marekani 1-1 Wales
Kundi C
Argentina 1-2 Saudi Arabia
Mexico 0-0 Poland
Kundi D
Denmark 0-0 Tunisia
Ufaransa 4-1 Australia
Kundi E
Ujerumani 1-2 Japan
Hispania 7-0 Costa Rica
Kundi F
Morocco 0-0 Croatia
