Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amesema timu yake bado ina nafasi kubwa ya kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kufanya vizuri mechi tano zilizobaki.
Simba jana Jumamosi ilianza vibaya mechi za hatua ya makundi ya michuano hiyo baada ya kufungwa bao 1-0 na Horoya AC wakiwa ugenini Conakry, Guinea.
Robertinho amesema sababu kubwa iliyopelekea timu yake kupoteza mchezo huo ni uchovu uliotokana na safari ndefu kutoka Dar es Salaam hadi Guinea ambapo walitumia zaidi ya saa 12.
“Uchovu umechangia kutofanya vizuri lakini nimeridhishwa na kiwango kilichooneshwa na wachezaji wangu hasa kipindi cha pili baada ya mabadiliko ya wachezaji watatu niliyoyafanya na tulipata nafasi tatu za wazi ndani ya eneo la hatari la mpinzani lakini hatukuzitumia vizuri,” alisema Robertinho.
Kocha huyo ameeleza kuwa mipango yake baada ya timu kurudi nchini ni kuandaa mkakati maalumu utakaowawezesha kushinda mechi zijazo ikiwamo ya wikiendi ijayo dhidi ya Raja Casablanca.
Robertinho alisema anajua Raja ni klabu kubwa lakini hata Simba ni kubwa hivyo mkakati uliopo mbele yao ni kuhakikisha wanashinda mchezo huo sababu watakuwa kwenye ardhi yao ya nyumbani tena mbele ya mashabiki wao watakaokuwa wanawapa sapoti.
“Nina imani kubwa tutashinda mchezo wetu ujao dhidi ya Raja, kutokana na mkakati tutakaoingia nao kwenye mchezo huo, nawaamini wachezaji wangu wana vipaji vikubwa lakini jana tuliwakosa baadhi ya wachezaji wetu akiwemo Saido Ntibazonkiza huyo ni mchezaji muhimu kwangu, mchezo ujao atakuwepo,” alisema Robertinho.
Alisema kwenye hatua hiyo ya mashindano hakuna timu ndogo hivyo wamejipanga kucheza kwa umakini mkubwa hasa katika mechi zao za nyumbani ili kuhakikisha wanashinda mechi zote na kusonga mbele hatua inayofuata.
Simba inatarajiwa kurejea nchini kesho Jumattu ikitokea Guinea na kwa mujibu wa viongozi, timu hiyo, itafikia kambini kuhakikisha inashinda mchezo huo ili kuweka hai matumaini yao ya kutinga robo fainali ya michuano hiyo mikubwa kwa ngazi za klabu Afrika.
Simba imepangwa Kundi C ambalo mbali na Raja na Horoya, pia lina timu za Vipers ya Uganda, timu ambayo Robertinho alikuwa akiinoa kabla ya kutua Simba.
