Tokyo, Japan
Mwanariadha wa Tanzania, Felix Simba amepongezwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kushinda medali ya dhahabu katika mashindano ya riadha ya dunia ya Tokyo akimshinda Amanal Petros wa Ujerumani katika ushindani uliokuwa mkali baina yao.
Katika salamu zake za pongezi zilizopatikana kwenye mitandao ya kijamii, Rais Samia alimpongeza Simbu kwa ushindi huo alioupata Jumatatu hii Septemba 15, 2025, akisema mwanariadha huyo ameandika ukurasa mpya katika historia ya Tanzania.
Rais Samia alisema mwanaridha huyo alishauriwa kuongeza bidii zaidi baada ya kutwaa medali ya shaba katika mbio za Marathon za Boston Aprili mwaka huu na sasa amefanya hivyo Tokyo kwa kushinda medali yenye hadhi ambayo ni ya dhahabu.
Alisema kwamba mwanariadha huyo amekuwa mfano kwa wanariadha wengine na kumtaka kuendelea kuongeza bidii zaidi.
Kwa upande wa Simbu ushindi wake haukuwa rahisi kwani yeye na mpinzani wake wa karibu katika mbio hizo za Marathon ambazo ni za kilomita 42, walimaliza pamoja wakitumia muda wa saa mbili, dakika nne na sekunde 48.
Simbu, 33, hata hivyo picha zilimuonesha akiwa amemzidi kwa viungo vya mwili katika mstari wa mwisho na hivyo akatangazwa moja kwa moja kuwa mshindi.
Katika picha hizo, Petros aliyeshinda medali ya fedha alionekana kuwania ushindi kwa kutanguliza kichwa lakini mkono na goti la Simbu vilionekana kumzidi kidogo na hivyo Simbu kuibuka kinara wa mbio hizo zenye hadhi ya kimataifa.
Nafasi ya tatu katika mbio hizo ilikwenda kwa mwanariadha wa Italia, Illias Aouani ambaye alipewa medali ya shaba, alimaliza mbio hizo kwa kutumia muda wa saa mbili, dakika tisa na sekunde 53.
Mbio hizo za Marathon zilishirikisha wanariadha 88 kutoka nchi 47 ambapo wanariadha walikuwa wakishindana kwa umbali wa kilomita 42 katika mitaa ya jiji la Tokyo nchini Japan huku wanariadha 22 wakishindwa kumaliza umbali huo kutokana na matatizo mbalimbali.
Kimataifa Simbu atwaa dhahabu Tokyo, Rais Samia ampongeza
Simbu atwaa dhahabu Tokyo, Rais Samia ampongeza
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
