Na mwandishi wetu
Wakati Yanga ikiwa njiani kuifuata Rivers United nchini Nigeria kwa ajili ya mechi ya kwanza ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, kocha wa timu ya taifa ya Uganda, Milutin Sredojevic ‘Micho’ ameipa nafasi Yanga ya kutinga nusu fainali ya michuano hiyo.
Micho )pichani) alisema kwa uzoefu alionao kwa timu za Afrika, anaiona nafasi ya Yanga kufuzu nusu fainali kwa asilimia 75 kutokana na mabadiliko makubwa waliyoyafanya kikosini.
“Nafuatilia kwa karibu soka la Tanzania, Yanga imebadilika sana, najua wametoka kupoteza mchezo dhidi ya Simba lakini hiyo haiwezi kuwa sababu ya kufanya vibaya kwa namna walivyojipanga na ubora waliokuwa nao hivi sasa,” alisema Micho.
Micho aliyewahi kuinoa Yanga alisema mshambuliaji Fiston Mayele mwenye muendelezo mzuri wa kufunga, anaamini ataendelea kuibeba timu hiyo sambamba na nyota wengine ambao wameivusha Yanga tangu hatua za mwanzo.
“Sasa hivi Khalid Aucho kwenye eneo la kiungo ni mchezaji bora sana katika ukanda huu lakini pia wana kipa (Djigui Diarra) ambaye ana uwezo mkubwa hata wa kuipanga timu na kuanzisha mashambulizi naweza kusema wametimia,” alisema Micho.
Yanga itaivaa Rivers Jumapili hii, kabla ya kurudiana Aprili 30, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam na timu itakayofuzu hapo itakutana na mshindi wa mechi kati ya Pyramids ya Misri na Marumo Gallants ya Afrika Kusini.
