Na mwandishi wetu
Yanga imezidi kuizamisha Prisons kwenye Ligi Kuu NBC baada ya kuinyuka mabao 3-0 katika mechi iliyochezwa Jumamosi Aprili 4, 2026 kwenye dimba la KMC, Mwenge, Dar es Salaam.
Matokeo hayo yanazidi kufifisha matumaini ya Prisons kucheza ligi hiyo msimu ujao kwani hiyo inakuwa mechi ya tano mfululizo kwa timu hiyo bila kupata ushindi na katika mechi 18 ilizocheza imeambulia pointi 13 na inashika nafasi ya 15.
Kwa upande wa Yanga matokeo hayo yanazidi kuiimarisha timu hiyo katika msimamo wa ligi ikiwa kileleni na pointi zake 41 baada ya kuingia dimbani mara 17.
Prisons iliuanza mchezo kwa kuonesha umakini ikishambulia na kujihami vizuri na haikushangaza katika dakika 45 za kwanza hakuna timu iliyoliona lango la mpinzani wake.
Kipindi cha pili Yanga ilikianza kivingine na kufanikiwa kuzichana nyavu za Prisons katika dakika ya 50 kwa bao lililofungwa na Allan Okelo aliyeitumia krosi ya Israel Mwenda.
Yanga iliendelea kulisakama lango la Prisons na kuongeza bao la pili dakika ya 68 lililofungwa na Mudathir Yahya baada ya kushirikiana vyema na Okello wakati bao la tatu lilifungwa na Pazome Zouzoua dakika ya 87 akiitumia pasi ya Duke Abuya.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo, Namungo walikuwa wenyeji wa JKT Tanzania na timu hizo zilimaliza dakika 90 kwa sare ya mabao 2-2.
Kimataifa Yanga yazidi kuizamisha Prisons
Yanga yazidi kuizamisha Prisons
Related posts
Read also
