Na mwandishi wetu
Mabeki wa kati wa Yanga, Ibrahim Bacca na Dickson Job wamewaahidi mashabiki wao kupambana kutafuta ushindi kwenye mechi yao dhidi ya Simba, hivyo wajitokeze kwa wingi siku ya mechi hiyo, Jumapili hii.
Bacca (pichani juu) alisema kama wachezaji wako vizuri kuelekea mchezo huo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam na wanaendelea kupokea maelekezo muhimu kutoka kwa makocha wao, hivyo kilichobaki ni kuongezewa morali ya mashabiki siku hiyo ili kuongeza mapambano ya ushindi.
“Mpaka sasa tuko vizuri kama wachezaji lakini walimu wetu wanazidi kutuongezea vitu kuelekea mechi hiyo, tuna morali na tuko vizuri kwa mapambano na kikubwa tunawaahidi ushindi mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi kwani hii ni timu yao.
“Uwepo wao ndipo jitihida zetu zitakapoongezeka pindi tukiwaona wamejitokeza, ni mchezo mgumu kila mtu anaelewa hilo lakini kama wachezaji tushaondoa hiyo hofu na tuko tayari kuukabili mchezo huo,” alisema Bacca.
Naye Job alisema: “Tunaamini ni jukumu lao lakini tungewaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi kutupa sapoti kwani tunaamini kuja kwao kwa wingi uwanjani ndio kutatupa morali na kupambana kwa dakika 90 na kuwapa furaha.
Katika mechi hiyo, mbali na upinzani uliopo baina ya timu hizo lakini pia kuwania nafasi ya kushika usukani wa ligi kunanogesha upinzani wa mechi hiyo.
Timu hizo zitaingia uwanjani zikiwa na pointi 18 lakini Yanga iko juu kutokana na uwiano mzuri wa mabao ya kufunga huku ikiwa imecheza mechi saba wakati Simba imecheza sita mpaka sasa na inashika nafasi ya pili.