Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi ameeleza kukerwa na tabia ya wachezaji wa Kagera Sugar ya kujiangusha katika dakika za mwisho na kupoteza muda, akidai kitendo hicho kimewanyima mashabiki kuufurahia mchezo huo.
Mchezo huo uliochezwa jana Ijumaa kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba na kuisha kwa suluhu inakuwa mechi ya kwanza kwa Yanga kuondoka na pointi moja msimu huu.
Gamondi alisema kipindi cha kwanza kilikuwa na presha kubwa lakini ngwe ya pili walicheza vizuri na kutengeneza nafasi kadhaa japo haikutosha kuwapa ushindi na kupata pointi tatu.
“Dakika 15 za mwisho wachezaji wa Kagera Sugar walikuwa wanajiangusha sana na kupoteza muda, sio nzuri kwa mpira wa Tanzania kwani mpira wa miguu ni mchezo wa matokeo unaweza kushinda, kufungwa na kutoka sare.
“Siwezi kumlaumu mwamuzi, alikuwa sahihi lakini kitendo cha kupoteza mpira kilishusha morali, kinachotakiwa tunapaswa kucheza kama mabingwa watetezi na kushinda michezo iliyo mbele yetu,” alisema Gamondi.
Naye Kocha Msaidizi wa Kagera Sugar, Marwa Chamberi, alisema: “Si jambo rahisi kuondoka na pointi moja mbele ya bingwa mtetezi lakini vijana walipambana na kufanikisha hilo, tunarudi kujipanga sasa kwa ajili ya mchezo ujao,” alisema Chamberi.