Na mwandishi wetu
Simba au Wekundu wa Msimbazi wameendelea kutambulisha wachezaji wao wapya iliowanasa kwa ajili ya msimu ujao na safari hii ni zamu ya kiungo mshambuliaji, Augustine Okrah kutoka Bechem United ya Ghana.
Kiungo huyo raia wa nchini Ghana ametambulishwa na Wekundu hao Jumatano hii akielezwa kupewa mkataba wa miaka miwili.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally ameeleza kuwa mchezaji huyo ni wa kiwango cha juu, wakiamini kuwa ataisaidia timu hiyo msimu ujao kutokana na uwezo alionao baada ya msimu uliomalizika timu hiyo kushindwa kutamba.
Okrah ambaye amekuwa akitajwa kutua Msimbazi kwa muda mrefu kabla ya kutambulishwa muda mfupi uliopita ameondoka Bechem baada ya kuisaidia kuipeleka timu hiyo fainali ya Kombe la FA kabla ya kufungwa mabao 2-1 na Hearts of Oak.
Katika kombe hilo, Okrah amecheza mechi tano na kufunga mabao matatu, pia aliifungia mabao 14 katika mechi 32 alizocheza na kuiwezesha timu hiyo kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi nyuma ya Medeama na mabingwa Asante Kotoko.
Okrah ambaye pia amewahi kukipiga BK Hacken ya Sweden, Smouha (Misri), Al-Merrikh (Sudan) na Asante Kotoko pia msimu wa 2013/14 aliibuka mchezaji bora wa Ligi Kuu Ghana akifunga jumla ya mabao 16 wakati akiitumikia Bechem.
Usajili huo ni usajili wa tatu wa wachezaji wa kimataifa kutangazwa na Simba baada ya Mzambia, Moses Phiri na Mnigeria, Victor Akpan. Wachezaji wazawa ni Nassoro Kapama kutoka Kagera Sugar na Habibu Kyombo kutoka Mbeya Kwanza.
Soka Okrah atambulishwa Simba
Okrah atambulishwa Simba
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
