Manchester, England
Kocha wa Man United, Erik ten Hag amemwambia mshambuliaji wake Marcus Rashford kwamba kama akiendelea na juhudi na umakini anaouonyesha sasa ataweza kuendelea kufunga mabao.
Kasi ya mabao ya mshambuliaji huyo imekuwa kivutio tangu kumalizika kwa fainali za Kombe la Dunia ambapo ameweza kufunga mabao sita mfululizo ikiwamo juzi Jumanne alipofunga mabao mawili katika mechi dhidi ya Charlton ambayo Man United ilitoka na ushindi wa mabao 3-0.
Nyota huyo wa timu ya Taifa ya England, hadi sasa amefikisha mabao 15 ikiwa ni mabao 10 zaidi ya yale aliyofunga msimu uliopita wakati kama huu na ni saba pungufu ya mabao 22 aliyoyafunga katika msimu wake unaotajwa kuwa bora wa 2019-20.
“Anapojipanga vizuri katika eneo la ‘box’ ataendelea kufunga na hicho ndicho anachokifanya kwa sasa, akiwa makini na kuwa mwenye kuendelea kufanya juhudi ataendelea kufunga,” alisema Ten Hag.
Keshokutwa Jumamosi, Rashford atakuwa na kazi nyingine ngumu ya kudhihirisha ubora wake wakati Man United itakapoumana na Manchester City kwenye Uwanja wa Old Trafford.
Ten Hag akizungumzia mechi hiyo aligusia majeraha ya misuli yanayomkabili Diogo Dalot ambaye huenda akaikosa mechi yao na Man City.
Dalot, beki wa kulia wa Man United aliumia kipindi cha kwanza kwenye mechi na Charlton na kutolewa kama tahadhari na Aaron Wan-Bissaka kuchukua nafasi yake ingawa jana Jumatano jopo la madaktari wa Man United lilikuwa likimfuatilia kwa karibu kujua ukubwa wa maumivu aliyonayo.
Kimataifa Ten Hag ampa neno Rashford
Ten Hag ampa neno Rashford
Read also