Manchester, England
Kwa mara nyingine kocha wa Man United, Erik ten Hag amemkingia kifua beki na nahodha wa timu hiyo, Harry Maguire akisema ni mchezaji wa mfano kwa wachezaji wengine kwenye timu.
Mara kadhaa Maguire amekuwa akibebeshwa zigo la lawama kutokana na kiwango chake cha uchezaji lakini Ten Hag ameendelea kumuamini na hajawahi kuwa tayari japo kumvua unahodha wa timu hiyo.
Alhamisi iliyopita, Maguire alishushiwa lawama kwa makosa aliyoyafanya katika mechi na Sevilla na kuwa sababu mojawapo ya timu hiyo kutolewa kwenye Europa Ligi.
Beki huyo anadaiwa kusababisha bao la mapema la Sevilla huku kiwango chake kikiwa mjadala kwa mara nyingine baada ya Man United kulala kwa mabao 3-0 na hivyo kutolewa katika michuano hiyo kwa jumla ya mabao 5-2.
Ten Hag hata hivyo anaonekana kuwa tofauti akisema kwamba Maguire mwenye umri wa miaka 30 anaendelea kuwa mtu muhimu kwenye kikosi chake.
“Maguire ana jukumu muhimu kwenye timu, ndiye nahodha, anaongoza wenzake, anawasiliana na kocha anaishawishi timu, ni mchezaji wa mfano katika mazoezi,” alisema Ten Hag.
Maguire si mchezaji pekee aliyeshushiwa lawama baada ya matokeo mabaya dhidi ya Sevilla, hali ambayo pia iliibua hoja ya uwezekano wa wachezaji walio wengi kuachwa baada ya msimu ingawa Ten Hag amesema anaangalia hali ya sasa katika kikosi chake.
“Nafikiria kuhusu kuiboresha timu hii na wachezaji hawa hawa, hiyo ndiyo kazi yangu na jopo la makocha na wachezaji, fikra zetu zote zipo katika mchakato huo na si mchakato mwingine ambao utatutoa kwenye mstari,” alisema.
“Najua kundi hili la wachezaji linaweza kufanya vizuri, wamethibitisha hilo mara nyingi katika msimu huu, tumepiga hatua kubwa katika msimu huu japo ni kweli kuna hatua za kuchukua, tuna mechi nyingi za kucheza na tunatakiwa kuthibitisha ubora,” aliongeza.
Man United, leo Jumapili ina mechi ya nusu fainali ya Kombe la FA dhidi ya Brighton & Hove Albion kwenye dimba la Wembley na Ten Hag amesema kwamba timu yake inatakiwa kuwa na mtazamo imara na kujifunza kutorudia makosa yaliyowakwanza katika mechi zao.