London, England
Kocha mpya wa Aston Villa, Unai Emery ana kila sababu ya kufurahia ushindi wake wa kwanza leo Jumapili wa mabao 3-1 dhidi ya Man United katika Ligi Kuu England wakati kocha Erik ten Hag amesema kwamba matokeo hayo hayakubaliki.
Ushindi huo wa nyumbani pia unakuwa ni jambo kubwa kwa Aston Villa kwani unafuta rekodi mbovu ya mechi 23 bila ushindi katika mechi zao dhidi ya Man United.
“Tulipoteza mchezo mara tu baada ya kuanza kipindi cha kwanza pamoja na kipindi cha pili, na hilo halikubaliki, walionekana kuwa freshi na wenye utayari, tunahitaji kuwa wepesi, matokeo yako wazi hayaongopi, leo hatukuwa vizuri kiasi cha kutosha,” alisema Ten Hag.
“Hatukujipanga vizuri, tulitengeneza nafasi nzuri wakati tukiwa 2-1 lakini inakatisha tamaa kuona tunapoteza mchezo mara tu baada ya kuanza kipindi cha pili, hili halikubaliki, ilikuwa haraka mno kwenye kipindi cha pili kwa shambulizi la kushitukiza,” aliongeza Ten Hag.
Wenyeji Villa waliandika bao lao la kwanza katika dakika ya saba tu ya mchezo huo lililofungwa na Leon Bailey aliyeizidi ujanja safu ya ulinzi ya Man United kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa, David de Gea.
Dakika tatu baadaye, Villa iliandika bao la pili lililofungwa na Lucas Digne kwa mpira wa adhabu wa umbali wa mita 25 na kuwaacha wachezaji wa Man United wakiwa wameduwaa wasiamini kilichotokea kabla ya kupata bao lao pekee ambalo Jacob Ramsey alijifunga wakati akiokoa mpira uliopigwa na Luke Shaw muda mfupi kabla ya timu hizo kwenda mapumziko.
Kipindi cha pili Man United iliingia na matumaini ya kusawazisha na kuongeza bao lakini iliduwazwa
dakika nne tu baada ya kipindi hicho kwa bao lililofungwa na Ramsey aliyesawazisha kosa lake na kutosha kuifanya Villa itoke na ushindi.
Ushindi huo wa Villa pia unakuwa jambo baya kwa Cristiano Ronaldo ambaye kwa mara ya kwanza chini ya Ten Hag alipewa jukumu la unahodha.
Kwa Villa ambayo ilimtimua kocha Steven Gerrard na nafasi yake kukabidhiwa Emery Oktoba 24, ushindi huo sasa unaifanya timu hiyo ichupe hadi nafasi ya 13 ikijiondoa kwenye janga la timu zinazohofiwa kushuka daraja
Matokeo ya mechi za EPL leo Jumapili…
Chelsea 0-1 Arsenal
Aston Villa 3-1 Man Utd
Southampton 1-4 Newcastle
West Ham 1-2 Crystal Palace
Tottenham 1-2 Liverpool
Matokeo ya mechi za EPL jana Jumamosi…
Leeds United 4- 3 Bournemouth
Man City 2 -1 Fulham
Nottingham 2-2 Brentford
Wolves 2-3 Brighton
Everton 0-2 Leicester
