
Munich, Ujerumani
Kipa wa Bayern Munich, Manuel Neuer amesema kwamba aliugua maradhi ya saratani ya ngozi na kulazimika kufanyiwa upasuaji mara tatu.
Neuer ametoa kauli hiyo leo Jumatano ambapo amesema alikuwa na kovu karibu na pua na madaktari kumfanyia upasuaji mara tatu baada ya kuathiriwa na maradhi hayo ingawa hakusema ni lini alifanyiwa operesheni hiyo japo alionekana kwenye picha akiwa ameweka plasta katika eneo lililoathirika.
Kipa huyo hakuonekana akiichezea timu hiyo tangu Oktoba 8 alipoumia bega lakini klabu ya Bayern imedai kuwa anaweza kupata nafasi na kuiwakilisha timu hiyo Jumamosi ijayo kwenye mechi dhidi ya Hertha Berlin.
Neuer ambaye ameichezea timu ya Taifa Ujerumani mara 113, aliisaidia timu hiyo kuibuka vinara wa taji la Dunia mwaka 2014 nchini Brazil na anatarajiwa kuwamo katika kikosi cha timu hiyo ambacho kitaenda Qatar kwenye fainali za Kombe la Dunia.
