Na mwandishi wetu
Hatimaye Yanga imefuzu hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza baada ya kuilaza Marumo Gallant ya Afrika Kusini mabao 2-1 katika mechi iliyopigwa leo Jumatano kwenye Uwanja wa Royal Bafokeng, Afrika Kusini.
Yanga inakuwa imefuzu hatua hiyo kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-1 baada ya ushindi wa mabao 2-0 iliyoupata katika mechi ya nusu fainali ya kwanza iliyopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam.
Timu hiyo sasa inasubiri kuumana na mshindi wa mechi nyingine ya nusu fainali iliyozikutanisha Asec Mimosa na USM Alger ambazo katika nusu fainali ya kwanza iliyopigwa mjini Abidjan timu hizo zilitoka sare.
Yanga iliandika bao la kwanza dakika moja kabla ya mapumziko mfungaji akiwa Fiston Mayele ambaye anakuwa amefikisha mabao sita katika michuano hiyo na kujiweka pazuri katika kuwania tuzo ya mfungaji bora.
Mayele ambaye baadaye alitolewa na kuingia Farid Mussa, alifunga bao hilo kwa pasi ya Musonda, kwanza alifumua shuti ambalo liliokolewa na kipa Washington Arubi wa Marumo kabla ya kumkuta mfungaji aliyemalizia kwa kuujaza wavuni.
Marumo ambao waliutawala mchezo huo kwa kiasi kikubwa, walijikuta wakifungwa bao la pili katika dakika ya 68 lililofungwa na Kennedy Musonda ambaye aliitumia vizuri pasi ya Mayele.
Mayele kabla ya kutoa pasi iliyozaa bao aliambaa na mpira na kumzidi mbio beki wa Marumo kabla ya kumuunganishia Musonda aliyeujaza wavuni akifumua shuti karibu na eneo la 18.
Marumo ambao kwa muda wote huo walikuwa wakimiliki vyema mipira na kufika mara kwa mara langoni mwa Yanga walichanganywa na bao hilo kwani lilikuja wakati wameonyesha uhai katika kutafuta bao la kusawazisha.
Bao pekee la Marumo lilipatikana katika dakika nne za nyongeza mfungaji akiwa ni Ranga Chivaviro ambaye sasa anakuwa amefungana na Mayele kwa idadi ya mabao kila mmoja akiwa n mabao sita.
Kimataifa Yanga hiyooo, fainali Shirikisho
Yanga hiyooo, fainali Shirikisho
Read also