Na mwandishi wetu
Klabu ya soka ya Yanga imeendelea kushikilia msimamo wake wa kutocheza mechi yao ya Ligi Kuu NBC dhidi ya mahasimu wao Simba iliyopangwa kuchezwa Juni 15, mwaka huu.
Uamuzi huo umeendelea kusisitizwa kabla na hata baada ya kikao cha viongozi wa klabu hiyo na wale wa bodi ya ligi kilichofanyika Jumatatu hii, Juni 9, 2025.
Kabla ya kikao hicho kilichofanyika kwenye ofisi za bodi ya ligi jijini Dar es Salaam, mashabiki na wapenzi wa klabu hiyo mitaani na kwenye mitandao ya kijamii walishikilia msimamo huo ambao baadaye ulipata baraka za viongozi wao.
Taarifa ya klabu ya Yanga iliyotolewa baada ya kikao hicho ilithibisha kushiriki kikao hicho na kuweka wazi kuwa uamuzi wao kwenye kikao umeendelea kuwa ule ule wa kutocheza mechi hiyo.
Katika msimamo huo Yanga wameweka wazi kwamba hawatacheza mechi hiyo hadi pale matakwa yao waliyoyawasilisha kwa maandishi yatakapotimizwa.
“Hatutashiriki mchezo namba 184 uliopangwa kufanyika tarehe 15 Juni, 2025 mpaka pale matakwa yetu tuliyowasilisha kwao kwa maandishi yatakapotimizwa,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo ya Yanga.
Uamuzi huo unazidi kuiweka pagumu mechi hiyo ambayo suala lake lilifika hadi kwenye vikao vya Bunge huku baadhi ya wabunge wanaodhaniwa kuwa ni mashabiki wa Yanga wakipaza sauti zao kusisitiza kuwa timu yao haitacheza mechi hiyo.
