Paris, Ufaransa
Kocha wa timu ya PSG ya Ufaransa, Luis Enrique amesema timu yake inahitaji kujiandaa na maisha bila ya mshambuliaji wao tegemeo, Kylian Mbappe anayetarajia kuondoka baada ya msimu huu.
Enrique ni kama vile ameanza kulifanyia kazi jambo hilo Jumapili hii baada ya kumtoa nahodha huyo wa Ufaransa katika dakika ya 65 kwenye mechi dhidi ya Rennes iliyoisha kwa sare ya 1-1 na nafasi yake kuingia Goncalo Ramos.
Ramos ambaye aliingia PSG ikiwa nyuma kwa bao 1-0, hakumuangusha kocha wake baada ya kufunga bao la kusawazisha kwa mkwaju wa penalti katika dakika za lala salama.
“Ni jambo rahisi tu, ni hivi sasa au hapo baadaye itakapotokea ni lazima tuzoee kucheza bila ya Kylian, nitakapotaka kumchezesha nitamchezesha, nisipotaka sitofanya hivyo,” alisema Enrique alipoulizwa kuhusu uamuzi wa kumtoa Mbappe.
Mwezi uliopita zilikuwapo habari kwamba Mbappe aliwaarifu mabosi wa PSG kuhusu nia yake ya kuihama timu hyo na inadaiwa hadi sasa yuko kwenye mazungumzo na klabu ya Real Madrid.
Hii ni mara ya pili kwa Enrique kumzungumzia Mbappe, aliwahi kufanya hivyo wiki mbili zilizopita alipotakiwa kutoa maoni kuhusu kuondoka kwa mchezaji huyo lakini alikataa akisema kwamba atatoa kauli yake baada ya pande mbili husika kuzungumza.
“Ninataka kumaliza suala hili, sina cha kusema, pande husika hazijasema chochote hadharani, Kylian Mbappe hajasema lolote hadharani, pindi pande mbili zitakapozungumza nami nitatoa maoni yangu,” alisema Enrique.