Manchester, England
Kasi ya ushindi wa Arsenal katika Ligi Kuu England hatimaye imegonga mwamba Jumapili hii baada ya kuchapwa mabao 3-1 na Manchester United katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Old Trafford.
Kabla ya mechi ya leo ambayo ni ya sita tangu kuanza kwa ligi hiyo, Arsenal ilikuwa timu pekeeambayo haikupoteza wala kutoka sare mchezo wowote ikiwa tayari imejikusanyia pointi 15 na michezo mitano lakini sasa inabaki na pointi 15 katika mechi sita ingawa bado inaongoza ligi hiyo.
Man Utd ina kila sababu ya kuufurahia ushindi huo ambao umeisimamisha Arsenal, timu ambayo iliianza ligi kwa kasi lakini pia inajivunia winga wake mpya Mbrazil, Antony ambaye mechi ya leo ni ya kwanza kwake akiwa na jezi ya Man Utd na ameianza kwa kupata bao.
Antony ambaye amejiunga na timu hiyo kwa ada ya uhamisho ya Pauni 82 milioni akitokea Ajax aliandika bao la kwanza la timu hiyo katika dakika ya 35 akiitumia vizuri pasi ya Marcus Rashford lakini Bukayo Saka wa Arsenal alifufua matumaini kwa timu yake aliposawazisha bao hilo katika dakika ya 60. Furaha ya mashabiki wa Arsenal hata hivyo ilidumu kwa dakika sita tu baada ya Rashford kuongeza bao la pili kwa Man Utd lililotokana na shambulizi la kushitukiza kabla mfungaji hajaunasa mpira kutoka kwa Bruno Fernandes na kuujaza wavuni.
Dakika 10 baadaye Rashford aliongeza bao la tatu, safari hii akiitumia pasi ya Eriksen kuhitimisha ushindi muhimu kwa timu yake, ushindi ambao umevuruga rekodi ya Arsenal kushinda mechi zake zote tangu kuanza kwa ligi.
Awali Gabriel Martinelli aliipatia Arsenal bao kipindi cha kwanza lakini baada ya kuangaliwa picha za VAR mwamuzi alilikataa bao hilo.
Akizungumzia matokeo hayo, kocha wa Arsenal, Mikel Arteta alisema, “Mchezo ulikuwa wa kushinda, hatukushinda kwa sababu tulikosa nidhamu katika baadhi ya matukio na hatukuwa wasumbufu kiasi cha kutosha tulipokuwa mbele ya goli.”
“Tukicheza kwa ujasiri zaidi tunashinda mechi, hili ni somo kubwa, kama unataka kushinda ni lazima ufanye kila kitu katika namna sahihi,” aliongeza.
Kwa upande wake kocha wa Man Utd, Erik ten Hag alisema kwamba timu yake imekuwa bora kifikra na ari imekuwa juu.
Kimataifa Kasi ya Arsenal yakwamia Old Trafford
Kasi ya Arsenal yakwamia Old Trafford
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
