Manchester, England
Mshambuliaji wa Man United, Marcus Rashford amesema hakupangwa kwenye kikosi kilichoanza mechi na Wolves kwa sababu alipitiwa na usingizi hadi kuchelewa kwenye kikao cha maandalizi ya mechi hiyo.
Katika mechi hiyo iliyochezwa jana Jumamosi hata hivyo alikuwa ni Rashford aliyetokea benchi na kubadili matokeo baada ya kufunga bao pekee la ushindi la timu hiyo katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Molineux.
Rashford alitarajiwa kuwamo kwenye kikosi cha kwanza katika mechi hiyo baada ya kufunga mabao mawili katika mechi mbili zilizopita tangu kumalizika kwa fainali za Kombe la Dunia lakini katika hali ambayo haikutarajiwa jina lake halikuwamo kwenye kikosi cha kwanza.
Akizungumza baada ya mechi hiyo, Rashford mwenye umri wa miaka 25 hakutaka kuficha sababu ya adhabu hiyo aliyopewa na kocha wake Eric ten Hag ya kunyimwa namba kwenye kikosi kilichoanza aliposema ni taratibu za timu na alifanya kosa.
“Hizo ni taratibu za kwenye timu, nilikosea na hilo hutokea, ukweli ni kwamba imenihuzunisha kwa kutocheza timu iliyoanza lakini naelewa uamuzi huo na nina furaha kwa sababu tumeweza kupata ushindi,” alisema Rashford.
“Tuliweka taratibu na tukakubaliana katika hilo lakini nilichelewa kidogo kwenye kikao, nilipitiwa na usingizi lakini ni jambo la kawaida ambalo hutokea,” alisema.
Rashford ambaye amekuwa katika kiwango kizuri msimu, amesema timu ipo tayari kuwa katika ubora baada ya mambo kuwa hovyo msimu uliopita, “Nafikiri niko vizuri, navutiwa jinsi tunavyopiga hatua, siku za nyuma tulikuwa tunapoteza mechi kirahisi au kupata sare.”
Naye kiungo wa timu hiyo kutoka Brazil, Casemiro alimpongeza Rashford kwa kucheza kwa kiwango cha juu na kuongeza kwamba anaweza kuwa mmoja wa wanasoka bora dunia, “niwe mkweli, navutiwa na uchezaji wa Rashford, naweza kusema akiendelea hivyo anaweza kuwa mmoja wa wachezaji watano bora duniani.”
Matokeo ya Jumamosi ya mechi za ligi hiyo ni kama ifuatavyo…
Wolves 0-1 Man United
Bournemouth 0-2 Crystal Palace
Fulham 2-1 Southampton
Man City 1-1 Everton
Newcastle 0-0 Leeds
Brighton 2-4 Arsenal
