Na mwandishi wetu
Baada ya kulala kwa mabao 5-1 mbele ya mahasimu wao Yanga, Simba leo Alhamisi imejikuta ikilazimisha sare ya bao 1-1 kwa Namungo FC katika mechi ya Ligi Kuu NBC.
Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, Namungo ndio waliokuwa wa kwanza kuzitikisa nyavu za Simba dakika ya 28 kwa bao la Reliant Lusajo, bao ambalo lilidumu hadi timu zinakwenda mapumziko.
Baada ya kuingia bao hilo, Simba ilipambana ikitaka kusawazisha lakini ilikumbana na upinzani wa Namungo hadi katika dakika ya 75 ilipopata bao lililofungwa na Jean Baleke.
Matokeo hayo yanaifanya Simba kubaki nafasi ya pili kwenye ligi hiyo ikiwa na pointi 19 sawa na Azam lakini Simba inaneemeka na wastani mzuri wa mabao wakati Namungo inashika nafasi ya 12 ikiwa na pointi nane.
Yanga ndiyo inayoshika usukani ikiwa na pointi 24 baada ya kucheza mechi tisa lakini Simba imecheza michezo minane hadi sasa.
Kocha wa Namungo, Denis Kitambi ambaye kabla ya mechi hiyo alinukuliwa akisema kwamba Simba inafungika na kuahidi kutumia nafasi hiyo kupata ushindi, baada ya mechi alijifariji akisema kwamba japo walikuwa na nafasi ya kushinda lakini matokeo ya sare si mabaya.
Kwa upande wake kocha wa muda wa Simba, Daniel Cadena alisema kwamba wana wajibu wa kufanya bidii ili kushinda mechi zao zijazo za ligi.
Soka Simba yalazimisha sare kwa Namungo
Simba yalazimisha sare kwa Namungo
Read also