Na mwandishi wetu
Kipa wa Yanga, Djigui Diarra amefungiwa mechi tatu na kutozwa faini ya Sh milioni mbili kwa kumshambulia mwamuzi wa mechi ya Ligi Kuu NBC kati ya Yanga na Mtibwa Sugar baada ya mchezo huo kumalizika kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
Katika mechi hiyo hiyo iliyoisha kwa sare ya bao 1-1, Diarra pia ametozwa faini ya Sh milioni mbili kwa kosa la kuonesha ishara ya kidole cha kati wakati akitoka uwanjani.
Taarifa ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) iliyopatikana Ijumaa Machi 27, 2026 ilieleza kuwa uamuzi huo umefikiwa na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya bodi hiyo iliyopitia mwenendo wa matukio mbalimbali ya ligi.
Mwamuzi wa kati wa mchezo huo, Gilbert Mrina wa Kilimanjaro ameshushwa daraja kwa kushindwa kumchukulia hatua stahiki Diarra kwa kuonesha utovu wa nidhamu, Mrina pia anadaiwa kufanya kosa kama hilo akiwa mwamuzi wa kati wa mechi ya Namungo na Mbeya City.
Naye mwamuzi msaidizi namba mbili wa mechi ya Yanga na Mtibwa, Abdulaziz Ally wa Arusha amefungiwa mizunguko mitano ya ligi hiyo kwa kushindwa kutafsiri vyema sheria za soka.
Inadaiwa katika dakika ya 36, Ally alinyoosha juu kibendera kuashiria kulikuwa na kosa la kuotea kabla ya mchezaji wa Yanga, Emmanuel Mwanendo kupokea pasi ya Pacome Zouzoua ingawa kimsingi hakukuwa na kosa hilo.
Katika adhabu nyingine, klabu ya Simba nayo imetozwa faini ya Sh milioni 10 kwa kosa la mashabiki wake kuwarushia chupa za maji waamuzi wa mchezo wao na Pamba Jiji uliomalizika kwa sare ya bao 1-1.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, tukio hilo ni la pili kufanywa na mashabiki wa Simba katika kipindi cha miezi miwili, kabla ya hapo mashabiki hao walimrushia chupa hizo mchezaji wa Dodoma Jiji, William Edgar wakati mchezo baina ya timu hizo ukiendelea.
Katika tukio jingine, timu ya TRA United imetozwa faini ya Sh 500,000 kwa kosa la wachezaji wao kupewa kadi za njano zaidi ya tano katika mechi yao na Yanga ambapo jumla ya kadi sita zilitolewa kwa wachezaji wa timu hiyo.
Soka Diarra afungiwa mechi tatu
Diarra afungiwa mechi tatu
Read also
