Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Maxime amesema ana imani kubwa na mshambuliaji Anuar Jabir ‘Falcao’ (pichani) aliyekwenda kufanya majaribio kwenye klabu ya Gent inayoshiriki Ligi Kuu Ubelgiji.
Mshambuliaji huyo amefika Ubelgiji leo Jumanne kwa ajili ya ofa hiyo inayotarajia kumweka nchini humo kwa wiki mbili na kama benchi la ufundi la Gent likiridhishwa naye basi wataanza mazungumzo na Kagera.
Maxime ameiambia GreenSports leo kuwa anaamini sasa kauli yake ya ‘hutaki hela’ ndiyo inaleta maana kwani mara ya kwanza ilitafsiriwa tofauti wakati akimpigia kelele kwa kauli hiyo mchezaji huyo kwenye mechi dhidi ya Azam iliyoisha kwa sare ya mabao 2-2.
“Nafikiri ingerejewa sasa ile kauli yangu ya hutaki hela maana wakati ule kuna watu walikurupuka na kunitafsiri tofauti lakini nilikuwa namaanisha kama hiki kinachoendelea sasa juu yake.
“Niseme kwamba hapa tumemwona mzuri ndio maana tulikuwa tunampa nafasi ina maana na kama wao wamemuona ina maana ana kitu kama sisi tulivyokuwa tukimwona, hivyo tunamwombea heri wakione vizuri alichonacho na mwisho afanikiwe,” alisema Maxime.
Wakati huohuo, uongozi wa Kagera Sugar leo umetangaza kuvunja mkataba wa miaka miwili na kiungo Abdul Aziz Makame baada ya kuitumikia timu hiyo kwa msimu mmoja.
Kupitia taarifa hiyo iliyowekwa kwenye kurasa za mitandao ya kijamii ya klabu hiyo, imeonesha kumshukuru na kumtakia heri mchezaji huyo katika maisha yake mapya ya soka aendako bila ya kutaja sababu ya kuvunja mkataba huo.
