Roma, Italia
Kocha wa Roma, Jose Mourinho amesema kwamba anafikiria kutafuta msaada wa kisheria akidai ‘alijazwa hasira’ na mwamuzi msaidizi katika tukio ambalo alijikuta akipewa kadi nyekundu.
Tukio hilo lilitokea wakati Roma ikiumana na Cremonese, timu inayopambana kujinasua isishuke daraja lakini ilipata ushindi wa mabao 2-1 ambao ni ushindi wa kwanza kwa timu hiyo.
Matokeo hayo yameivuruga Roma ambayo imejikuta ikiangukia nafasi ya tano katika Ligi Kuu Italia au Serie A na hivyo kutolewa katika mbio za kuwania kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Mourinho ambaye alipewa kadi hiyo muda mfupi baada ya kuanza kipindi cha pili na kuondoka katika benchi, alisema chanzo cha kadi hiyo ni mwamuzi msaidizi. Ni kadi nyekundu ya tatu kwa Mourinho katika msimu huu wa Serie A.
“Kwa mara ya kwanza katika kazi yangu ya ukocha mwamuzi ananizungumzisha katika namna isiyo nzuri,” alisema Mourinho katika mkutano na waandishi wa habari baada ya mechi hiyo.
“Mimi si kichaa, na nilifanya nilichofanya kwa sababu ya kilichojitokeza, najaribu kuangalia kama naweza kufanya kitu katika mtazamo wa kisheria,” alisema Mourinho, kocha wa zamani wa Chelsea, Inter Milan, Real Madrid, Man United na FC Porto.
“Mwamuzi wa kati (Piccinini) alinipa kadi nyekundu kwa sababu msaidizi wake alimwambia afanye hivyo lakini mwamuzi msaidizi pia hawezi kumwambia alichoniambia mimi, alichonifanyia na kunifanya nikasirike,” alisema Mourinho.