Na mwandishi wetu
Benchi la ufundi la Yanga limeeleza kuwa tayari kwa mchezo wao wa Jumamosi hii dhidi ya Mbeya City ingawa itamkosa kiungo wake tegemeo, Feisal Salum ‘Fei Toto’ kutokana na kuwa na kadi tatu za njano.
Pamoja na hayo, taarifa njema kwa vinara hao wa ligi ni kurejea kwa wachezaji wao waliokuwa kwenye majukumu ya timu za taifa, Stephane Aziz Ki wa Burkina Faso na kipa Djgui Diarra raia wa Mali.
Akizungumza leo, Kocha Msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze alisema hata hivyo kikosi hicho katika mechi hiyo kinatarajia kuwa na sura mpya kwa ajili ya kupumzisha wachezaji wengine kutokana na mfululizo wa mechi za mwezi Novemba walizokuwa nazo.
Yanga itaikaribisha Mbeya City kwenye Uwanja wa Mkapa, jijini Dar es Salaam ikiwa imetoka kushinda mabao 2-0 dhidi ya Dodoma Jiji wakati Mbeya ikitoka kupapatuana na Simba katika mechi iliyoisha kwa sare ya bao 1-1.
“Siwezi kusema kama tuna muda wa kujiandaa sana maana tumetoka kucheza Jumanne, tumerudi hapa na tumefanya mazoezi mepesi mepesi, tukijua pia tunaenda kukutana na mpinzani ambaye yuko vizuri, tunafahamu ugumu wa mechi lakini nasi tumejiandaa kiakili, fiziki na kimbinu zaidi.
“Kuna wachezaji watakosekana kesho (leo) kutokana na sababu mbalimbali, panapaswa kuwa na mabadiliko kutokana na mechi saba tulizocheza tangu Novemba Mosi hivyo tutafanya mabadiliko lakini hayataathiri uwiano wa timu.
“Kuna wachezaji wengine wamerudi pia kutoka kwenye majukumu ya timu za taifa, Aziz Ki na Diarra. Bangala (Yanick) ambaye naye alikuwa na adhabu amerudi ila Fei Toto atakosekana kutokana na kuwa na kadi tatu za njano,” alisema Kaze.
Mbali na mechi hiyo, mechi nyingine wikiendi hii ni Ruvu Shooting inayonolewa na Charles Mkwasa itakuwa kibaruani kuikabili Singida Big Stars ya Hans Pluijm katika mchezo utakaopigwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Soka Yanga iko tayari kuikabili Mbeya City
Yanga iko tayari kuikabili Mbeya City
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
