Na mwandishi wetu
Kocha mkuu wa Kagera Sugar, Fred Minziro ameahidi kuiondolea timu hiyo unyonge na kuirudisha kwenye ushindani kama ilivyokuwa hapo awali.
Akizungumza na GreenSports, Minziro alisema hiyo ni kutokana na wachezaji waliopo kuwa na uwezo mkubwa wa kushika haraka anachofundisha kwenye mazoezi.
“Nataka kuirudisha Kagera Sugar ya zamani ambayo iliogopwa hata na timu vigogo na hilo linawezekana kutokana na aina ya wachezaji nilionao kwenye kikosi changu, wana uwezo mkubwa wa kushika ninachowaelekeza,” alisema Minziro.
Alisema mechi mbili walizocheza katika uwanja wa nyumbani wa Kaitaba na kuvuna pointi nne zimempa mwanzo mzuri wa kutimiza kile ambacho amekiahidi kwa uongozi na mashabiki wa timu hiyo.
Alisema kwa kuwa ameichukua timu hiyo ikiwa nafasi za chini kwenye msimamo, mikakati yake ni kushinda mechi zote watakazocheza nyumbani huku wakitafuta sare au ushindi mechi za ugenini.
Kagera Sugar chini ya Minziro imepata ushindi wake wa kwanza wa bao 1-0 dhidi ya Singida Fountain Gate na kupanda hadi nafasi ya 10 kwenye msimamo wa Ligi Kuu NBC wakiwa na pointi 17.
Soka Minziro kuondoa unyonge Kagera
Minziro kuondoa unyonge Kagera
Read also