Rio de Janeiro, Brazil
Brazil itacheza mechi mbili za kirafiki na timu za Afrika kama sehemu ya kupiga vita visa vya ubaguzi wa rangi anavyokumbana navyo mshambuliaji wa Real Madrid na timu ya Brazil, Vinicius Junior.
Vinicius amekuwa akikumbana na kadhia za ubaguzi wa rangi katika Ligi Kuu Hispania ‘La Liga’ jambo ambalo limewafanya mabosi Shirikisho la Soka Brazil (CBF) kuingilia kati kwa kuandaa mechi hizo.
Brazil ambao ni mabingwa wa dunia mara tano, watacheza na Guinea mjini Barcelona, Juni 17 na kufuatiwa na mechi ya pili dhidi ya Senegal ambayo itapigwa mjini Lisbon, Ureno, siku tatu baadaye.
Mbali na mechi hizo, CBF pia wamedhamiria kuzindua kampeni ya kitaifa ya kupiga ubaguzi wa rangi kwenye ligi ya soka nchini humo wakianzia mechi za wikiendi hii baada ya Vinicius kukumbana na kadhia hiyo Jumapili katika mechi ya Real Madrid na Valencia.
Tukio la Jumapili linakuwa la 10 kwa Vinicius katika msimu huu pekee ingawa tayari mabosi wa La Liga wameshalifikisha suala hilo kwenye vyombo vya sheria nchini Hispania na baadhi ya watuhumiwa kukamatwa.
Katika kampeni za kupiga vita ubaguzi wa rangi nchini Brazil, CBF wamezindua kauli mbiu ya ‘hakuna mchezo wenye ubaguzi wa rangi’, kampeni ambayo ni sehemu ya mkakati ulioanzishwa mwaka 2022 na rais mpya wa CBF, Ednaldo Rodrigues.
Rodrigues kwa kipindi kirefu amekuwa akitaka kuona mamlaka za kisheria nchini Brazil zinatumia adhabu kali dhidi ya wahusika wa ubaguzi wa rangi kwenye viwanja vya soka.
“Tunataka Brazil iongoze vita ya ubaguzi wa rangi duniani kote,” alisema Rodrigues katika mahojiano aliyofanya na shirika moja la habari la kimataifa.