Na mwandishi wetu
Simba leo Jumapili imefanikiwa kuchelewesha safari ya Yanga kulitetea taji la Ligi Kuu NBC baada ya kuichapa mabao 2-0 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Simba iliuanza mchezo huo kwa kupata bao la mapema lililofungwa dakika ya pili ya mchezo na beki wake wa kati, Henock Inonga kwa kichwa aliporuka juu kuuwahi mpira mbele ya mabeki wa Yanga.
Wakati Yanga ikipambana kusawazisha bao hilo ilijikuta ikifungwa bao la pili dakika ya 32 mfungaji akiwa Kibu Dennis aliyefumua shuti kali la mbali baada ya kuwazidi ujanja mabeki wa Yanga na mpira kumshinda kipa Diarra.
Baada ya kuona mambo si mazuri kocha wa Yanga, Nassredine Nabi alifanya mabadiliko kwa kuwatoa wachezaji watatu, akawaingiza Mudathir Yahya, Aziz Ki na Tuisila Kisinda kuchukua nafasi za Bangala, Salum Aboubakar na Moloko.
Mabadiliko hayo licha ya kuipa Yanga uhai kwa kulisakama lango la Simba katika kipindi cha pili lakini timu hiyo haikuweza kuzichana nyavu za Simba ambazo katika mechi ya leo zililindwa na kipa Ali Salim ambaye mara nyingi amekuwa ni mchezaji wa akiba wa timu hiyo.
Matokeo ya mechi ya leo yanakuwa yameichelewesha safari ya Yanga kuutangaza ubingwa mapema kwani sasa watalazimika kufanya hivyo baada ya kushinda mechi tatu kati ya tano zijazo ambapo kama wangeshinda leo wangekuwa na nafasi ya kuutangaza ubingwa katika mechi mbili zijazo.
Yanga na Simba zote zimebakiwa mechi nne kabla ya kumaliza ligi huku Yanga ikiwa kileleni na pointi zake 68 wakati Simba inashika nafasi ya pili na pointi 63.

Hiyo maana yake ni kwamba kama Yanga watashindwa kuzitumia vizuri mechi mbili zijazo na Simba kuzitumia vizuri, huo utakuwa mwanzo wa kujiweka pabaya kwani watashushwa kileleni na Simba na vita yao kuhamia katika mechi mbili za mwisho.
Mazingira hayo yanaweza kuwa na faida kwa Simba ambao ikitokea timu hizo kufungana pointi, mwisho wa siku timu hiyo inaweza kuneemeka na mabao mengi ya kufunga. Yanga ina mabao 50 ya kufunga wakati Simba ina mabao 60.
Ushindi wa leo pia una maana kubwa kwa Simba kwani umekuja baada ya timu hiyo kunyanyaswa na Yanga katika mechi za ligi za miaka ya karibuni.
Simba licha ya kuwa na rekodi nzuri ya kubeba taji la ligi kuu kwa misimu takriban minne iliyopita lakini imekuwa ikikwama mbele ya Yanga kwa ama kufungwa au kuambulia sare, mara ya mwisho kupata ushindi dhidi ya Yanga katika mechi za ligi hiyo ilikuwa Februari 2019 iliposhinda kwa bao 1-0.
