Leipzig, Ujerumani
Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola amesema kwamba aliwakusanya wachezaji wake uwanjani baada ya sare ya bao 1-1 na RB Leipzig kwa sababu hakufurahishwa na unyonge waliokuwa nao.
Man City jana Jumatano usiku ikiwa ugenini ilitoka sare hiyo katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya 16 bora jambo lililowatia huzuni wachezaji wa timu hiyo na kuonekana wakiwa vichwa chini mara baada ya filimbi ya kumaliza mchezo kupulizwa.
Katika mechi hiyo Man City ilikuwa ya kwanza kupata bao lililofungwa dakika ya 27 na Riyad Mahrez kabla ya kukatishwa tamaa na bao la kusawazisha lililofungwa dakika ya 70 na Josko Gvardiol.
Man City iliutawala mchezo katika dakika 45 za awali kabla mambo hayajawaharibikia kipindi cha pili lakini Pep aliwafuata wachezaji wake na kuwakumbusha kwamba alifurahia kiwango chao.
“Walikuwa vichwa chini, niliwafuata na kuwaambia kwa nini mnakuwa vichwa chini, muwe na furaha, hakika mmecheza katika kiwango kizuri, kama watu hawajapenda hiyo haijalishi,” alisema Pep.
“Mechi ilikuwa nzuri hasa, tulicheza vile tulivyotakiwa kucheza, walikuwa wepesi na walicheza kwa kasi, hatukuwa katika kasi hiyo, tulitawala mchezo kipindi cha kwanza, tulitengeneza nafasi, walifunga njia, bado tuna mechi Manchester na tutaona nani atashinda,” alisema.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyochezwa jana, Inter Milan iliichapa FC Porto bao 1-0.