Na mwandishi wetu
Yanga imeshika usukani wa Ligi Kuu NBC baada ya kuinyuka Namungo FC mabao 3-1 katika mechi iliyopigwa Ijumaa hii jioni kwenye Uwanja wa Majaliwa mjini Ruangwa, Lindi.
Ushindi huo unaifanya Yanga kufikisha pointi 46 ikiiacha Azam FC iliyo nafasi ya pili kwa tofauti ya pointi mbili ingawa Azam imecheza mechi tatu zaidi ya Yanga.
Yanga hata hivyo ilibidi ifanye kazi ya ziada kupata matokeo katika kipindi cha pili baada ya kuhaha kusaka bao kwa kipindi chote cha kwanza lakini hadi dakika 45 zinakamilika ubao ulisomeka 0-0.
Bao la kwanza la Yanga lilipatikana dakika nane baada ya kuanza kipindi cha pili mfungaji akiwa ni Mudathir Yahya ambaye aliitumia vizuri pasi ya Stephanie Aziz Ki.
Mambo yalizidi kuwaharibikia Namungo dakika tatu baadaye walipojikuta wakifungwa bao la pili mfungaji akiwa Clement Mzize ambaye alifunga goli hilo kwa shuti dhaifu.
Mzize alipata bao hilo baada ya kuyatumia makosa ya beki wa Namungo, Derick Mkombozi aliyekuwa akitaka kumpiga chenga mshambuliaji huyo lakini mpango huo ulifeli na ukazaa bao la pili kwa Yanga.
Mambo yaliendelea kuwaharibikia Namungo dakika tatu zilizofuata walipofungwa bao la tatu mfungaji akiwa ni Aziz Ki ambaye aliitumia pasi ya Yao kufunga bao hilo.
Namungo ilipata bao lao pekee la kufutia machozi dakika ya 71 ambalo ‘walizawadiwa’ na beki wa Yanga Ibrahim Bacca ambaye alijifunga wakati akijaribu kuokoa krosi ya Emmanuel Charles.
Soka Yanga yaiengua Azam kileleni
Yanga yaiengua Azam kileleni
Read also
