Na mwandishi wetu
Baada ya Taifa Stars kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2024, Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kuna haja kwa timu hiyo kuanza maandalizi mapema ili iende kupambana na si kushiriki kama ilivyokuwa huko nyuma.
Stars ilifuzu fainali hizo kwa mara ya tatu kufuatia matokeo ya suluhu na vinara wa Kundi F, Algeria katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Mei 19, Annuba na kuziacha Uganda na Niger zikikosa tiketi ya kushiriki fainali hizo zitakazofanyika Ivory Coast, mwakani.
Akizungumza wakati akifunga kikao cha Bunge mjini Dodoma leo Ijumaa, Majaliwa alisema kufuzu Afcon ni jambo zuri lakini itapendeza zaidi endapo kutakuwa na mikakati itakayoiwezesha timu hiyo kufanya vizuri ili kuzidi kuitambulisha Tanzania kimataifa.
“Leo nina furaha kubwa sana kwa Taifa Stars kufuzu fainali za Afcon baada ya kutoka suluhu na Algeria, naitakia kila la heri katika michuano hiyo, nawapongeza sana wachezaji kwa kupambana kupigania taifa lao.
“Haikuwa kazi rahisi hata kidogo kutokana na ubora waliokuwa nao Algeria lakini vijana hawakukubali kuona wanaipoteza nafasi hiyo, tunafurahi lakini wahusika wanapaswa kuandaa timu hii mapema ili twende tukapambane na siyo kushiriki,” alisema Majaliwa.
Majaliwa pia aliwataka Watanzania kuiunga mkono timu hiyo ili iendelee kuleta matokeo mazuri kwenye fainali hizo zitakazoanza Januari, mwakani.
Mbali na Majaliwa pia baadhi ya makocha wazawa nao wameshauri kuanza mapema kwa maandalizi ya michuano hiyo wakiamini bado kuna kazi kubwa kuelekea michuano hiyo ya 34 tangu kuanzishwa kwake.
Kocha wa zamani wa Stars, Boniface Mkwasa alisema: “Nawapongeza kwa kweli wachezaji na benchi la ufundi kwa suluhu waliyoipata maana mchezo ulikuwa mgumu, kitu cha msingi ni maandalizi mazuri sababu kufuzu Afcon ni rahisi lakini kushiriki mashindano yenyewe ndio kuna ugumu zaidi. Kingine kocha anapaswa kuchagua wachezaji wenye ubora ambao ndio atakwenda nao kwenye fainali.”
Naye Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ ambaye ni kocha wa timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 23, kwanza alimpongeza Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ambaye jana ameipa Stars Sh milioni 500 kama zawadi ya kufuzu, kwa juhudi na jitihada zake za kuhamasisha michezo nchini hadi timu hiyo kufuzu.
“Nawapongeza sana wachezaji na benchi la ufundi, mchezo dhidi ya Algeria haukuwa rahisi kocha alichagua mpango sahihi wa kujihami ndio maana tukapata tulichokitaka, naamini tunaweza kuwashangaza wengi kama timu hii itapata muda wa kupiga kambi Ulaya itamsaidia kocha kujenga timu imara zaidi ya tuliyoiona juzi,” alisema Julio.
Abdallah Kibadeni, kocha na mchezaji wa zamani wa Simba, mchezaji pekee aliyewahi kufunga ‘hat-trick’ kwenye mechi ya Simba dhidi ya Yanga, alisisitiza ili kufanya vizuri kunahitajika maandalizi kabambe ikiwemo kucheza mechi za kirafiki za mataifa makubwa yaliyopo juu ya Tanzania kwa ubora.
“Nampongeza Kocha Mkuu, Adel Amrouche ameonesha uwezo mkubwa katika kumsoma mpinzani lakini furaha hii tuliyokuwa nayo inapaswa kuendelea, TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) na Serikali watumie muda huu kuiandaa timu ili kuhakikisha tunafika angalau robo fainali mwakani,” alisema Kibadeni.