Barcelona, Hispania
Barcelona imeahidi kufanya uchunguzi wa matukio ya ubaguzi wa rangi anayodaiwa kufanyiwa mshambuliaji wa Real Madrid, Vinicius Junior jana Jumamosi timu hizo zilipokutana katika El Clasico.
Katika mechi hiyo, Real Madrid walitoka na ushindi wa mabao 2-1, mabao ya washindi mfungaji akiwa Jude Bellingham wakati bao pekee la Barca likifungwa na Ilkay Gundogan.
Baada ya mechi hiyo ilielezwa kwamba Vinicius Jr ambaye alifanyiwa mabadiliko dakika za nyongeza, alikumbana na vitendo vya ubaguzi wa rangi kutoka kwa mashabiki wanaoaminika kuwa wa Barca.
Taarifa ya Barca iliyopatikana kwenye mitandao ya kijamii ilieleza kuwa klabu hiyo inalifanyika kazi tukio hilo linalowahusisha baadhi ya watu waliomfanyia Vinicius dhihaka za kibaguzi na baadaye watawasilisha mashtaka yanayohusiana na jambo hilo kwenye mamlaka.
“Wakati wote FC Barcelona italinda maadili ya soka na michezo ikiwamo heshima kwa timu pinzani na tutachunguza dhihaka zozote za ubaguzi wa rangi zinazojitokeza,” ilielea taarifa ya Barca.
Vinicius wiki iliyopita aliipongeza klabu ya Sevilla kwa kumfikisha kwenye vyombo vya sheria shabiki aliyejihusisha na matukio ya ubaguzi wa rangi dhidi yake.
Msimu uliopita Vinicius katika mechi hiyo pia alikutana na kadhia hiyo na huo kuwa mwendelezo wa dhihaka hizo dhidi yake jambo ambalo limelifanya Shirikisho la Soka Brazil (CBF) kuingilia kati kumtetea mchezaji huyo ambaye pia anaichezea timu ya taifa ya Brazil.
Septemba mwaka jana baadhi ya mashabiki wa Atletico Madrid kabla ya mechi yao na Real Madrid, walionekana wakiimba nyimbo za kuhamasisha ubaguzi wa rangi dhidi ya Vinicius nje ya uwanja wa klabu hiyo.
