Na mwandishi wetu
Simba imefuzu kwa mbinde nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi ikitoka na ushindi mwembamba wa bao 1-0 mbele ya Jamhuri katika mechi iliyopigwa Jumatatu hii usiku kwenye dimba la Amaan Complex.
Bao hilo pekee la Simba lilipatikana katika dakika tatu za nyongeza (dakika ya 46) kabla ya timu kwenda mapumziko mfungaji akiwa Jean Baleke aliyeujaza mpira wavuni kwa kichwa akiitumia krosi ya Miquissone.
Mpira uliozaa bao hilo ulianzia kwa Ngoma ambaye baada ya kuwazidi ujanja mabeki wa Jamhuri akiwa upande wa kushoto alipiga pasi ndefu ya mbali iliyomkuta Miquissone aliyekuwa upande wa kulia na kumuunganishia Baleke.
Baleke akitokea mbali aliwapita kwa kasi katikati mabeki wa Jamhuri na kuruka juu kabla ya kuupiga mpira huo kichwa na kumshinda kipa Nassir Talib Khamis.
Juhudi za Simba kutaka kuongeza mabao zilishindwa kuzaa matunda kutokana na umakini wa safu ya ulinzi ya Jamhuri ikiongozwa na kipa wao ambaye aliwawekea ngumu Simba licha ya mashambulizi ya mara kwa mara.
Katika harakati za kusaka bao, Baleke akiwa anaelekea kuonana na kipa wa Jamhuri, beki wa timu hiyo, Salum Said Ramadhan alimvaa kwa miguu miwili yeye na mpira hali iliyomlazimu mwamuzi kumpa beki huyo kadi ya njano.
Baada ya kuona ugumu wa kuongeza mabao, kocha wa Simba Abdelhak Benchikha aliwatoa Saido Ntibazonkiza na kumuingiza mchezaji wake mpya Sarr Babacar, akamtoa Baleke na kumuingiza Moses Phiri na Miquissone naye alitolewa na nafasi yake akaingia Saleh Kabaraka.
Mabadiliko hayo hata hivyo bado yalikumbana na ugumu wa timu ya Jamhuri ambayo wachezaji wake walicheza kwa kujihami zaidi na kufanya mashambulizi machache hali iliyowalazimu Simba kucheza pasi nyingi kwa lengo la kufungua uwanja lakini bado haikuwasaidia kupata bao.
Jamhuri bado kidogo wabadili matokeo katika dakika za 83 na 85 baada ya kufanya mashambulizi ya kushtukiza na kama si umahiri wa kipa Ayoub Lakred, timu hiyo ingeweza kupata mabao.
Katika mechi nyingine ya michuano hiyo iliyopigwa mapema jioni, Azam FC ilishindwa kutamba mbele ya Singida Fountain Gate baada ya kupokea kichapo cha mabao 2-1.
Soka Simba yafuzu kwa mbinde Mapinduzi Cup
Simba yafuzu kwa mbinde Mapinduzi Cup
Read also
