Na mwandishi wetu
Mshambuliaji wa Simba SC, Willy Onana amesema hana tatizo na kocha mkuu wa timu hiyo, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ na ana matumaini ya kufanya makubwa msimu huu akiwa na miamba hiyo.
Onana alisema hayo baada ya kudaiwa kuwa alichukizwa na kitendo cha kufanyiwa mabadiliko katika mchezo wa Ligi Kuu NBC dhidi ya Dodoma Jiji na nafasi yake kuchukuliwa na Moses Phiri, kitu kilichomfanya aondoke kwenye benchi na kuelekea kwenye vyumba vya kubadilishia nguo.
Nyota huyo raia wa Cameroon alisema hawezi kulumbana na kocha sababu anajua sheria za mchezo wa soka na anamheshimu sana Robertinho hivyo hata kuondoka kwake kwenye benchi ilikuwa ni kwa ruhusa yake.
“Kufanyiwa mabadiliko kwenye mpira ni jambo la kawaida na si mara ya kwanza kwangu, watu wajue sina tatizo na kocha Robertinho wala mchezaji au kiongozi yeyote wa timu.
“Ifahamike nina furaha sana tangu nijiunge na timu hii na imani yangu ni kwamba tutakuwa na msimu mzuri wenye mafanikio baada ya kubeba Ngao ya Jamii,” alisema Onana.
Mshambuliaji huyo ambaye tayari ameshafungua akaunti yake ya mabao akiwa na kikosi cha Simba alisema kwa muda mfupi ambao amecheza soka Tanzania amegundua ugumu na ushindani uliopo kwenye ligi hiyo ukilinganisha na ile ya Rwanda ambayo aliibuka mfungaji bora na mchezaji bora msimu uliopita.
Alisema malengo yake akiwa Simba ni kupambana kuipa timu hiyo ubingwa wa ligi kuu akishirikiana na wachezaji wenzake lakini pia wafike mbali kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Onana aliyesajiliwa Simba msimu huu akitokea Rayon Sports ya Rwanda ni kati ya wachezaji wanaotajwa kuleta ushindani mkubwa wa namba ndani ya kikosi cha Simba ambayo imepania kufanya vizuri msimu huu baada ya kushindwa kutwaa kombe lolote msimu uliopita.
Soka Onana: Sina tatizo na Robertinho
Onana: Sina tatizo na Robertinho
Read also